Dar es Salaam. Katika muktadha wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira, nishati safi imeendelea kuwa jambo la msingi kwa Taifa lolote linalotaka kupiga hatua kuelekea maendeleo endelevu.
Nchi inayokumbwa na changamoto za kiafya, mazingira na umaskini, nishati safi ya kupikia si tu hitaji la msingi, bali ni kichocheo cha maendeleo ya kweli kwa watu na Taifa kwa jumla.
Athari za matumizi ya nishati chafu si tu za kiuchumi bali hata kiafya na nyanja nyinginezo za kijamii.
Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), Tanzania hupoteza hekta 400,000 za misitu kila mwaka kutokana na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za misitu ikiwamo uvunaji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa hivyo, kuchangia kuongezeka kwa ukame nchini pamoja na athari za kiikolojia.
Ukataji huo wa miti ndio unatajwa na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) kuwa takribani asilimia 16 ya eneo la nchi tayari limegeuka kuwa jangwa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali ilizindua mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya watu wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa ifikapo mwaka 2034.
Katika kufanikisha mpango huo, mkakati huo umeweka bayana namna utakavyowezesha matumizi ya nishati safi kwa kuboresha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uzalishaji,upokeaji, uhifadhi na usambazaji wake.
Utekelezaji huo ni kwa kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia.
Taasisi za Serikali na utekelezaji
Katika kutekeleza mpango huo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia Meneja Masoko, Neema Cleophace wana miradi ambayo inaendelea kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kuwaunganisha wateja wapya 1,000 wa Mkoa wa Dar es Salaam gesi asilia.
Neema anasema TPDC ina miradi mingine inayoendelea kwa mwaka wa fedha wa fedha 2024/25 ya kuwaunganisha wateja 1,000 gesi asilia majumbani maeneo ya Lindi na Pwani.
Anasema hadi sasa nyumba 1,514 zimeunganishwa gesi asilia na mkoani Lindi hadi Mnazi Mmoja watu 209 wameunganishwa gesi asilia,Mtwara Bandari (125), Mtwara Kiyambu ( 300), Dar es Salaam Mikocheni (140),Kurasini (344),Sinza ( 221) na Mikocheni watu 72 huku viwanda 58 vikiunganishiwa nishati hiyo.
“Kutokana na ufanisi wake, gesi asilia ni ya gharama nafuu ukilinganisha na nishati nyingine kama vile mkaa, pia kutumia gesi asilia badala ya mkaa au kuni husaidia kupunguza ukataji miti na hivyo kulinda misitu na mazingira,”anasema.
Neema anasema matumizi ya gesi asilia kama nishati ya kupikia hupunguza uchafuzi wa hewa kwenye makazi na athari za kiafya zinazotokana na moshi.
Faida hizo za matumizi ya nishati safi anakiri Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Elizabeth Mbezi kuwa wanatumia nishati itokanayo na gesi, mkaa mbadala na gesi itokanayo na taka.
Anasema sababu kubwa ya jeshi hilo kugeukia kwenye matumizi ya nishati hizo ni unafuu wa upatikanaji wake kwa kuwa, ukataji wa kuni huchukua muda mrefu na matumizi yake husababisha maradhi.
“Gharama ya kuni ni kubwa, nishati mbadala ni nafuu zaidi,unapotumia moto wa kuni moshi ni mwingi na athari kiafya ni kubwa na hata kuni zenyewe huchukua muda mrefu upatikanaji wake, tulipoona changamoto hizo tukahamia kwenye nishati safi,”anasema.
Zabibu Rajabu, mkazi wa Mtwara ambaye ni mtumiaji wa nishati mchanganyiko (safi na chafu), anasema anashindwa kutumia aina moja ya nishati kutokana na upatikanaji.
Anakiri kuwa, mtumiaji wa gesi za mitungi akisema kwake ni salama kwa afya yake lakini anashindwa kuacha kutumia mkaa kwa kuwa, kujaza mtungi wa gesi ni gharama.
“Sipendi kutumia mkaa kila siku, napaswa kununua sado moja Sh1,500 natumia kwa siku moja na nusu, gesi nahitajika kuwa na Sh2,300 kujaza (majumbani), hela hii ni kubwa ni muhimu Serikali ikaangalia jinsi ya kutusaidia tumudu gharama za gesi,”anasema.
Zabibu anasema ipo gesi ya TPDC mkoani humo kama Serikali itashindwa kushushwa gharama za mitungi ya gesi kwa kuiwekea ruzuku ni muhimu bajeti ikatengwa kuunganisha wananchi na gesi asilia.
Kilio hicho hakitofautiani na cha Mariam Said mkazi wa Sabasaba mkoani Mtwara ambaye gesi kwao ni nzuri kwa afya na huarakisha mapishi tatizo ni gharama.
“Tunasomesha watoto asubuhi wanakwenda shule bila kupata chai, mkaa unawasha unazima hadi ukolee muda unapotea watoto wanaondoka, tuna mitungi tatizo kujaza ni gharama, kikwazo kikubwa kwangu napenda kutumia nishati safi ila kipato changu kidogo kujaza gesi,”anasema.
Rais Samia Suluhu Hassan Februari mwaka huu baada ya kuzindua awamu ya pili ya mradi wa ugawaji wa mitungi 452,000 ya gesi kwa wananchi mkoani Tanga,aliahidi Serikali kuja na mkakati wa kuleta unafuu wa matumizi ya nishati kwa kuweka ruzuku.
Ruzuku hiyo kwa mujibu wa Rais Samia, inahusisha kugharimia asilimia 50 ya bei ya mtungi wa gesi, huku mwananchi akichangia asilimia 50 kwa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wa vijijini, alisema Serikali inatoa ruzuku ya asilimia 20, huku mwananchi akichangia asilimia 80 ya bei ya mtungi huo kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Mtaalamu wa afya ya binadamu, Dk Ernest Winchislaus anasema moshi unaotokana na kuni,mkaa, mabaki ya mazao, matairi huwa na sumu akitolea mfano kabonimonoxide.
Anasema sumu zinazotokana na nishati hizo husababisha magonjwa ya mfumo wa hewa, Pneumonia (hasa kwa watoto) ugonjwa sugu wa mapafu).
Pia, kikohozi sugu, kikohozi cha mkamba, saratani ya mapafu (hata kwa wasiotumia sigara),magonjwa ya watoto na kina mama,vifo vya watoto wachanga kutokana na upungufu wa oksijeni,uzito mdogo wa mtoto wakati wa kuzaliwa na matatizo ya mimba kwa wajawazito.
Dk Winchislaus anasema takribani watu milioni 2.4 hufa kila mwaka duniani kote kutokana na matumizi ya nishati chafu kwa kupikia akinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani 2022 (WHO).
“Vifo vine kati ya vitano hutokea kwa wanawake na watoto walio karibu na jiko,kaya bilioni 2.3 duniani bado hutegemea kuni, mkaa na mabaki ya mimea kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia (IEA 2023)”,anasema Dk Winchislaus.
Anasema kwa Tanzania zaidi ya asilimia 70 ya kaya hutumia kuni au mkaa kupikia kulingana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS/REPOA 2022).
Mtaalamu huyo anasema matumizi ya nishati safi hupunguza kwa zaidi ya asilimia 90 moshi hatari unaoingia ndani ya nyumba.
“Hupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito, magonjwa ya kupumua na mzigo kwa vituo vya afya,huzuia ukataji miti kupita kiasi (hasa kwa ajili ya kuni/mkaa), hupunguza uzalishaji wa gesi chafu zinazochangia mabadiliko ya tabianchi,”anaeleza.
Mchambuzi wa Masuala ya Mazingira, Dk Aidan Msafiri anasema nishati chafu hukaa hewani kwa zaidi ya miaka 90, hivyo ni muhimu kutumia nishati safi ya kupikia.
“Tunapoteseka na mabadiliko ya tabia ya nchi suluhu ni kupunguza hewa ya ukaa kwenye maji, ardhi na angani na njia mojawapo ya kupunguza ni matumizi ya nishati safi,”anasema.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.