Usichokijua kuhusu kupikia ubwabwa kwenye gesi

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Environment Foundation, Glory Shayo amesema kwamba kuna dhana potofu katika jamii kuwa ubwabwa unaopikwa kwa kutumia gesi hakina ladha nzuri kama kile kinachopikwa kwa kuni au mkaa, jambo ambalo si sahihi.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 11, 2025 katika mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ikiwa na mada inayohoji; “Nini kifanyike Watanzania watumie nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na afya zao? Shayo amesisitiza kuwa tofauti ya ladha ya chakula kutokana na aina ya nishati inayotumika ni ndogo mno na mara nyingi huchangiwa na mazoea tu ya jamii.

“Kunaweza kuwa na utofauti wa ladha ya chakula kwa kiwango kidogo, lakini sio kweli kwamba ukipikia kwenye gesi chakula hakiwi kitamu. Watu wanapinga kwa sababu wamezoea kuni au mkaa,” amesema Shayo.

Shayo, ambaye pia ni mama na mpishi mwenye uzoefu wa kutumia aina mbalimbali za nishati majumbani, ameeleza kuwa gesi ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, urahisi wa kutumia, na ufanisi wa kupika chakula haraka ukilinganisha na mkaa au kuni.

Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi kama gesi si tu yanaboresha maisha ya familia bali pia ni suluhisho kwa changamoto za kiafya na kimazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Governance Links, Donald Kasongi, ameweka wazi kuwa Taifa linapaswa kuwa na mkakati thabiti na wa kitaifa wa kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema ni muhimu kuanzia kwenye elimu kwa wananchi kuhusu faida za nishati safi, ili kuongeza uelewa na kuvunja mitazamo potofu iliyojengeka katika jamii.

“Watu wengi wanaposikia gesi, wanahisi ni bidhaa ya matajiri au biashara ya watu wachache. Ukweli ni kwamba kuna aina nyingi za nishati safi na tunahitaji kuwaelimisha wananchi kuhusu hilo,” amesema Kasongi.

Amehimiza kuwa ili kufanikisha mpango wa kitaifa wa mabadiliko ya nishati kufikia mwaka 2034, kunahitajika ushirikiano wa sekta zote wanahabari, Serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za fedha na jamii kwa ujumla.

Kasongi amesema kuwa mipango hiyo haina budi kuzingatia maisha halisi ya wananchi wa kawaida na kuwa shirikishi katika hatua zote.

Naye Dickson Shekivuli ambaye ni Meneja wa Programu wa Nature and Climate Danmission East Africa, amesema nishati ni nguzo ya maisha ya kila siku, akisema ni vigumu kuitenganisha jamii na matumizi ya nishati, hasa kwa shughuli za kiuchumi kama kupikia, ujenzi na uzalishaji viwandani.

“Nishati ni maisha. Hatuna namna ya kuzungumzia maendeleo bila kugusia nishati. Iwe ni kupika, kujenga barabara kwa kuchemsha lami au kuendesha viwanda, yote yanahitaji nishati,” amesema.

Shekivuli ameeleza kuwa kuna fursa kubwa ya ubunifu katika sekta ya nishati safi, akitolea mfano Indonesia ambako taka hutumika kuzalisha nishati.

Amependekeza Tanzania ichukue hatua kama hizo, hasa kwenye majiji makubwa kama Dar es Salaam na Mwanza ambapo taka ni nyingi na zinaweza kuwa rasilimali muhimu.

Shekivuli amesisitiza umuhimu wa kuunda ajira kupitia mnyororo wa thamani wa nishati safi kutoka kwenye uzalishaji, usambazaji hadi kwa watumiaji wa mwisho na kusema hatua hiyo inaweza kuwanufaisha zaidi vijana na wanawake.

Shekivuli pia ameiomba Serikali kufanya mapitio ya sera na tozo mbalimbali kwenye nishati kama gesi na umeme, ili kuzifanya ziwe nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.

Amesema gharama ya juu ni mojawapo ya vikwazo vikubwa vinavyowazuia watu wengi kuhama kutoka nishati chafu kama kuni na mkaa.

Katika mjadala huo, Mtaalamu wa Takwimu kutoka MCL, Halili Letea, ameeleza kuwa chini ya asilimia 10 ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi ya kupikia.

Amesema idadi kubwa ya wananchi bado wanategemea kuni na mkaa, hali inayotishia mazingira na afya za wananchi.

Kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Uhifadhi wa Mazingira 2022–2032, Letea amesema ekari 439,000 za misitu hukatwa kila mwaka kwa ajili ya nishati ya kupikia.

Ameongeza kuwa maeneo yanayoathirika zaidi ni yale ya Kanda ya Magharibi, ambako kasi ya ukataji miti ni kubwa.

“Hii hali inahatarisha ikolojia na ustawi wa vizazi vijavyo. Tunapoteza rasilimali muhimu kila mwaka. Nishati safi inapaswa kuwa kipaumbele cha Taifa,” amesema.

Mbali na athari za kimazingira, Letea ametaja madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya nishati chafu, akisema takriban watu 33,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Amesema kundi la wanawake linatajwa kuathirika zaidi kwa kuwa ndio watumiaji wakuu wa nishati hizo kwa kupikia na kutafuta kuni.

Letea ameeleza kuwa nishati safi hupimwa kwa vigezo mbalimbali ikiwemo ufanisi, usalama kiafya na kimazingira, upatikanaji, urahisi wa matumizi na gharama.

Amehimiza kuwa juhudi za kitaifa zinapaswa kuelekezwa kwenye kutimiza vigezo hivyo ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati bora kwa kila Mtanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disability, Michael Salari, amesema kuwa tafiti mbalimbali za kimataifa zinaonyesha kuwa takriban asilimia 90 ya watu wenye ualbino hufariki dunia kutokana na saratani ya ngozi.

Amesema chanzo kikuu cha hali hiyo ni athari za moja kwa moja za mionzi ya jua, ambayo huathiri kwa kiwango kikubwa watu wenye ualbino kutokana na ukosefu wa kinga ya asili ya ngozi.

Salari ameongeza kuwa hali hiyo inazidi kuwa mbaya kutokana na ukataji holela wa miti, ambao umepelekea kupungua kwa maeneo yenye vivuli vinavyoweza kuwalinda watu hao dhidi ya mionzi hatari ya jua.

“Kundi la watu wenye ualbino limekuwa likipata changamoto kubwa sana kunapotokea uharibifu wa mazingira na ukiangalia Tanzania asilimia 80 ya watu wenye ualbino wanapoteza maisha kutokana na uharibifu wa mazingira na matumizi ya nishati chafu,” amesema.

Amesema ukataji wa miti ovyo kunawaweka kwenye hatari ya kupata athari unaochangiwa na uharibifu wa mazingira.

“Tumeanza kutoa elimu ya kulinda mazingira ili kuwaepusha watu wenye ulemavu wa ngozi ili athari za uharibifu wa mazingira,” amesema.

Salari amesema ni muhimu Serikali kuongeza msukumo wa matumizi ya nishati safi vijijini kwani huko hali sio nzuri, huwapokea wagonjwa wa saratani wakiwa hatua ya juu zaidi hali ambayo chanzo chake ni uharibifu wa mazingira.