Dar es Salaam. Upande wa mashitaka umedai bado inaendelea na upelelezi katika kesi ya kuingilia mfumo wa benki na kuiba Sh2.3 bilioni inayomkabili raia wa Ghana, Valentine Kofi (45) na wenzake watatu.
Kutokana na upelelezi kutokukamilika, washtakiwa hao wataendelea kukaa rumande kwa siku 14 kuanzia leo hadi Agosti 25, 2025.
Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Agosti 11, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mwakamele ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
“Washtakiwa wapo mbele ya Mahakama yako na kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa, lakini upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika, hivyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Mwakamele.
Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 25, 2025.
Mbali na Kofi ambaye ni mkazi ya Mikocheni washtakiwa wengine ni Patrick Tarimo (34) mkazi wa Kibaha, Aisha Kagashe(40) mkazi wa Sinza na Idan Msuya(46) mkazi wa Mikocheni.
Wanakabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kuingilia mfumo wa benki na kuiba Sh2 bilioni ambazo ni mali ya benki ya ABC.
Katika shitaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Septemba Mosi, 2021 na Oktoba 25, 2021 ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi tisa za Afrika ambazo ni Ghana, Ivory Coast, Uganda, Zambia, Senegal, Cameroon, Ufaransa, Mali na Bukinafaso.
Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliongoza genge hilo kwa kuingilia mfumo wa African Banking Corporation of Tanzania Limited (Banc ABC) kwa lengo la kuiba Sh2 bilioni mali ya benki hiyo.
Shitaka la pili ni kuingilia mfumo wa benki, ambapo washtakiwa hao na wengine ambao hawajafikishwa mahakamani siku na maeneo hayo, waliingilia mfumo wa kompyuta wa benki hiyo na kudukua akaunti 160 za visa za malipo ya awali zilizopo katika benki hiyo na kusababisha benki hiyo ipate deni la Sh3.5 bilioni.
Shitaka la tatu ni wizi, tukio wanalodaiwa kulitenda Oktoba 24 na Oktoba 25, 2021 katika maeneo hayo, ambapo washtakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafikishwa mahakamani, waliiba Sh2 bilioni kupitia kadi ya visa ya malipo ya awali kutoka katika benki hiyo yenye namba ya utambulisho 486054 mali ya benki hiyo.
Shitaka la nne ni kutakatisha fedha, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Oktoba 24, 2021 na Februari 18, 2025 katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam pamoja na nchi hizo, washtakiwa kwa pamoja na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani hapo, walijipatia Sh2 bilioni mali ya benki hiyo, wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la wizi.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 13, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.