Watatu kortini wakidaiwa kumpiga ngumi mwenzao

Dar es Salaam. Fundi magari, Tibelius Mgonela (55) na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, jijini Dar es Salaam kujibu shtaka moja la shambulio la kudhuru mwili.

Mgonela mkazi wa Mbezi na wenzake wanadaiwa kumpiga ngumi tumboni na ubavuni mlalamikaji, Raju Pache (60) na kumsababishia maumivu ya mwili.

Karani wa Mahakama hiyo, Aurelia Bahati amewataja washtakiwa wengine ni Mohamed Waziri (42) mkazi wa Kimara na Augustino Francis (31), mkazi wa Tabata na wote ni mafundi magari.

Bahati amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya jinai ya mwaka 2025, mbele ya Hakimu Gladness Njau.

Akiwasomea shtaka lao, Bahati amedai kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 5, 2025 saa 10:05 alasiri eneo la Upanga, mtaa wa Fire, Wilaya ya Ilala.

Inadaiwa siku hiyo kwa makusudi, walimshambulia Raju Pache (60) mkazi wa Upanga kwa kumpiga ngumi sehemu mbalimbali za tumboni na mbavuni na kumsababishia maumivu.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kitendo hicho ni kosa na kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baada ya kusomewa shtaka linalowakabili washtakiwa hao walikana kutenda kosa hilo na hakimu Njau ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.