ZAIDI YA WAOMBAJI 62,000 WAKAMILISHA MAOMBI YA MIKOPO HESLB

:::::::::

Na Mwandishi Wetu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuwa hadi sasa waombaji 62,950 wamekamilisha na kuwasilisha maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kati ya jumla ya waombaji 107,059 waliojisajili katika mfumo rasmi wa bodi hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu hali ya uwasilishaji wa maombi ya mikopo kwa mwaka ujao wa masomo.

Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, waombaji hao ni kutoka katika ngazi mbalimbali za elimu zikiwemo stashahada, shahada ya kwanza, stashahada ya juu ya mafunzo ya sheria kwa vitendo, pamoja na shahada za uzamili na uzamivu.

“Takwimu hizi zinaonesha hamasa kubwa kutoka kwa wanafunzi waliomaliza elimu ya sekondari na wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya juu nchini,” alisema Dkt. Kiwia.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia amesema zaidi ya wanafunzi 1,000 wanatarajiwa kupata ufadhili wa *Samia Scholarship* kwa mwaka wa masomo ujao, ambapo hadi sasa wanafunzi 603 kati ya 889 waliowasilisha fomu, wamekamilisha hatua zote muhimu.

Akizungumzia bajeti ya mwaka huu, Dkt. Kiwia amesema kuwa Serikali imetenga Shilingi bilioni 916.5 kwa ajili ya mikopo itakayowanufaisha wanafunzi 252,773, wakiwemo wanafunzi 88,320 wa mwaka wa kwanza na 164,453 wanaoendelea na masomo yao.

PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCH MEDIA