694 wachaguliwa kufundisha shule za msingi

Dar es Salaam. Jumla ya walimu 694 wamechaguliwa kufundisha kwa kujitolea katika shule mbalimbali za msingi nchini, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya uhaba wa walimu katika ngazi ya elimu ya msingi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema walimu hao walichaguliwa kutoka kwenye kundi la waombaji waliotuma maombi kati ya Mei 17 na 30 mwaka huu.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa jana Jumatatu Agosti 11, 2025 na Katibu Mkuu wa Tamisemi, walimu waliokidhi vigezo wanatakiwa kuripoti kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye maeneo yenye shule walizoomba, kuanzia Agosti 18 hadi 31.

Katika kipindi hicho, watasaini mkataba wa ajira ya kujitolea na kupatiwa barua za kupangwa vituo vya kazi.

Hatua hii imeelezwa na Serikali kama mwendelezo wa juhudi za kuongeza idadi ya walimu ili kuendana na ongezeko kubwa la wanafunzi, hasa baada ya sera za elimu bure kuongeza mahudhurio shuleni.

Hata hivyo, uwiano kati ya walimu na wanafunzi bado ni changamoto kubwa katika baadhi ya maeneo.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na kilio kikubwa cha ajira miongoni mwa vijana, hususani walimu.

Hali hiyo imesababisha kuibuka kwa makundi mbalimbali yanayopigia kelele ajira, ikiwemo Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira Tanzania (Neto).

Serikali tayari imetangaza kuwa walimu wanaojitolea watapewa kipaumbele endapo nafasi za ajira za kudumu zitapatikana huku utekelezaji wa mwongozo wa ajira kwa wanaojitolea ukianza kutekelezwa Julai 1 mwaka huu.

Juni 2023, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa mwongozo wa walimu wa kujitolea unaolenga kuimarisha mfumo wa ajira na huduma stahiki kwa walimu wa kujitolea katika shule za awali, msingi na sekondari.

Mwongozo huo pia unasisitiza umuhimu wa walimu wanaojitolea kuwa na makubaliano rasmi na waajiri wao.

Wadau mbalimbali wa elimu wamepongeza hatua hii akiwemo Japhet Kilomo ambaye amesema hatua hiyo itasaidia kuinua kiwango cha taaluma nchini hasa katika shule ambazo zina uhaba mkubwa wa walimu.

“Pamoja na Serikali kuendelea kuajiri, bado kuna umuhimu wa kuwatumia walimu hawa ili kuendeleza ujuzi wao na kuisaidia jamii. Hii itaboresha elimu hasa maeneo yenye upungufu mkubwa wa walimu.

“Tunafahamu kuna shule unaenda unakuta hakuna mwalimu wa somo fulani au mmoja aliyepo anafundisha madarasa yote, sasa kama kuna hawa wanaongezwa naamini kuna kitu kinaenda kupatikana kwa sababu bado wana nguvu na ari ya kazi,” amesema Kilomo.

Mwalimu Mstaafu Rehema Masanja amesema walimu wa kujitolea ni msaada mkubwa, lakini ameitaka Serikali kuhakikisha wanapatiwa posho ya kujikimu ili kuwapa hamasa zaidi.

“Kujitolea ni uzalendo, lakini maisha yao pia lazima yaendelee. Ikiwezekana wapatiwe hata posho ya nauli au chakula hata kama wamepangiwa kufundisha katika shule zilizopo kwenye maeneo wanayoishi,” amesema.