Nairobi. Askari wa Polisi mwenye cheo cha Konstebo, Manasseh Ithiru, ameripotiwa kufariki dunia baada ya kudaiwa kusukumwa kutoka juu ya ghorofa na mwenzake, Sajenti Abubakar Said, wakati wa ugomvi uliotokea katika makazi ya mwanamke anayedaiwa kuwa mpenzi wao wa pembeni ‘mchepuko’.
Tukio hilo lililotokea Jumamosi katika eneo la Kitengela, Kaunti ya Kajiado nchini Kenya, linadaiwa kuhusisha ugomvi wa kimapenzi baina ya maofisa hao wawili.
Kwa sasa, Sajenti Said anashikiliwa na polisi katika Kituo cha Polisi cha Kitengela huku uchunguzi wa kina ukiendelea kufanywa kubaini chanzo kamili cha tukio hilo, pamoja na mazingira yaliyosababisha kifo cha Konstebo Ithiru.
Tovuti ya Tuko kutoka nchini Kenya imeripoti kuwa askari hao wawili walihusika kwenye ugomvi uliosababisha kifo cha mmoja wao baada ya kukutana katika nyumba ya mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa mpenzi wao.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maofisa hao walikutana katika chumba namba 416 cha jengo la Geoffrey Flats lililoko Kitengela, Kaunti ya Kajiado, nyumbani kwa mwanamke aitwaye Irene Wavinya (27), ambapo ugomvi ulizuka baada ya wote wawili kufika kwa nyakati tofauti bila taarifa.
Konstebo Manasseh Ithiru, inadaiwa alikuwa wa kwanza kufika katika makazi hayo, alikutana na Sajenti Abubakar Said aliyewasili muda mfupi baadaye.
Inadaiwa kuwa mzozo wa kimapenzi ulitokea kati yao, na katika hali ya kutoelewana, Sajenti Said anadaiwa kumsukuma Ithiru kutoka kwenye balcony ya ghorofa ya nne, hali iliyosababisha askari huyo kuanguka na kufariki dunia papo hapo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Citizen Digital, Konstebo Ithiru alikuwa anahudumu katika Kituo cha Polisi cha Kitengela, ilhali Sajenti Said anatajwa kuwa ofisa wa Kambi ya CIPU EPZ Athi River.
Jengo hilo la Geoffrey Flats linapatikana takriban kilomita tatu kusini mwa Kituo cha Polisi cha Kitengela, kando ya Barabara ya Deliverance.
Mwili wa marehemu, ambao ulikuwa na majeraha kadhaa hasa kichwani, umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Shalom.
Wakati huohuo, Sajenti Said pamoja na Irene Wavinya wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.