Dar es Salaam. Askari Polisi mwenye namba WP 10050, Julieth Moshi (30) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Moshi kutoka Kisarawe, amefikishwa mahakamani hapo leo Agosti 12, 2025 na kusomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo ameyakana mashtaka hayo.
Julai 28, 2025, watu wanane wakiwemo askari polisi watano walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Baada ya kusomewa mashtaka yake, aliunganishwa katika kesi ya jinai namba 18451 ya mwaka 2025 yenye washtakiwa wanane, ambao leo hii kesi yao iliitwa kwa ajili kutajwa.
Mbali na Moshi, washtakiwa wengine ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF.19931 Fredrick Malekela (45), mkazi wa Kilwa Road; E.4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54), mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54), mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus (47), mkazi wa Kisarawe na F.5092 Sajenti John Kaposwe (46), mkazi wa Kurasini.

Wengine ambao sio maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59), mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce (60), mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29), mfanyabiashara na mkazi wa Tabata.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha, kinyume na kifungu namba 333 na 335A na kifungu 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Awali, kabla ya kusomewa mashtaka hayo, wakili wa Serikali, Roida Mwakamele alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika na hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini baada ya kusikiliza kesi hiyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, 2025 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Katika mashtaka yao, wanadaiwa kuwa vibali hivyo, vimetolewa kati ya Desemba 5, 2024 hadi Aprili 4, 2025.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024, ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya walitengeneza nyaraka ya uongo ambayo ni kibali cha kumiliki silaha cha Desemba 5, 2024 chenye jina la Ahmed Ally, wakati wakijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili hadi la 13, washtakiwa wanadaiwa katika kipindi cha mwaka 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, walitengeneza vibali vya kumiliki silaha vyenye majina ya Ahmed Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdad Chakindo, Irfan Nafari, Gulam Abbas Najafi, Ismail Ismail na Salim Salim.
Shtaka la 14 hadi 16, washtakiwa hao wanadaiwa mwaka 2025 katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai walitengeneza nyaraka za uongo ambazo ni kibali cha kumiliki silaha chenye jina la Marwaan Habretsh, Maurice Kitiwe na Said Mohamed, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Wakati huohuo, kesi ya kukutwa akimiliki bastola tatu na risasi 26 bila kuwa na leseni inayomkabili Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF.19931 Fredrick Malekela (45) imetajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.
Malekela kutoka kambi ya Polisi Kilwa Road, anadaiwa kutenda makosa yake kati Novemba 30, 2024 hadi Julai 2025.
Kati ya mashtaka hayo manane yanayomkabili Malekela, matatu ni ya kughushi; matatu ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo; moja la kukutwa akimiliki silaha tatu na lingine ni la kumiliki risasi bila kuwa na leseni.
Hakimu Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, 2025 itakapotajwa.