Badru amvulia kofia Kocha Taifa Stars

KOCHA wa zamani wa timu za vijana za Azam FC, Mohamed Badru amepongeza kazi kubwa inayofanywa na kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, pamoja na benchi lake la ufundi katika michuano ya CHAN 2024 yanayoendelea ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Badru alisema kiwango kilichooneshwa na Stars hadi kutinga robo fainali ni cha kuridhisha na kinaashiria mwelekeo chanya wa maendeleo ya soka nchini.

“Tumeshuhudia timu ikicheza kwa nidhamu, umoja na mikakati ya wazi. Hii ni dalili nzuri kwamba tupo kwenye njia sahihi ya kukuza mpira wa miguu wa Tanzania,” alisema Badru.

Badru, ambaye pia aliwahi kuifundisha Gwambina FC na Mtibwa Sugar, alieleza tofauti na mataifa mengi ya Afrika yanayojenga nguvu kwa wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi, Stars imekuwa na msingi wa kikosi chenye wachezaji wanaocheza pamoja katika Ligi Kuu.

“Wachezaji wetu wanajuana vizuri, wamezoea mazingira, na hii imerahisisha mawasiliano na utekelezaji wa mikakati ya mechi,” aliongeza.

Kihistoria, Tanzania imeandika ukurasa mpya katika michuano ya CHAN kwa kuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya robo fainali, baada ya kushinda mechi tatu kati ya nne (moja mkononi) za hatua ya makundi.

Ushindi huo ni dhidi ya Burkina Faso kwa mabao 2-0, Mauritania 1-0 na Madagascar kwa mabao 2-1, imesalia mechi moja tu kukamilisha hatua hiyo ambapo itavaa na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jumamosi.

Kwenye takwimu za hatua ya makundi, Stars ambayo ipo kundi B, imefunga mabao matano na kuruhusu bao 1 pekee, ikiwa na pointi 9 kati ya 12. Hii ni rekodi bora zaidi kwa timu hiyo tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo 2009 ambapo hii ni mara ya tatu kushiriki.