CCM yakusanya zaidi ya Sh86 bilioni chini ya saa 24

Dar es Salaam. Ndani ya saa 24, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimekusanya zaidi ya Sh86 bilioni katika harambee iliyoanzishwa ya kuchangia shughuli za kampeni za urais na ujenzi wa chama hicho.

Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh56.3 bilioni zimelipwa papohapo, huku zaidi ya Sh30.2 bilioni ni ahadi zinazotarajiwa kulipwa na wadau, makada na washabiki wa chama hicho kwa siku zijazo.

Kampeni hiyo ilitangazwa Agosti 11 saa 7 mchana na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiwakaribisha wadau, wanachama na wafuasi wa chama hicho kukichangia.

Usiju wa leo, Agosti 12, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City ilikokuwa inafanyika harambee hiyo, saa 5:30 usiku, Dk Nchimbi ametangaza tayari zaidi ya Sh56.3 bilioni zimeshaingia kwenye akaunti iliyotajwa, huku zaidi ya Sh30.2 bilioni zikiahidiwa.

Hata hivyo, amesema harambee hiyo inaendelea hadi Oktoba 27, 2025 siku ya mwisho wa kampeni za uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Baada ya taarifa ya kiasi kilichokusanywa huku nyingine zikiendelea kuingia, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na kuwashukuru waliochangia, amesema chama hicho kina nafasi ya pekee katika historia ya Tanzania tangu kuzaliwa kwake kwani kimekuwa na dhima ya kisiasa na kiuongozi.

Amesema ni historia adhimu ya CCM, ila historia pekee haiwezi kuendesha chama, ndiyo maana kimekuwa kikisisitiza mshikamano wa wanachama wake.

“Chama kinahitaji kutunzwa, kulishwa, ni kama gari bila mafuta haliwezi kwenda. CCM kutunzwa kwake ni mshikamano wa wanachama wake, moyo na mawazo na vitendo, kadhalika rasilimali kupitia vitendo kama tulivyofanya leo,” amesema.

Amesema michango hiyo inakiwezesha chama hicho kuanza shughuli za kwenda kuomba ridhaa ya kuomba nafasi ya kujenga dola wakati mwingine.

Amesema kilichotokea ni uthibitisho kuwa chama kitajengwa na wanachama na kwamba michango hiyo inawapa matumaini kuwa watakamilisha kampeni kwa mafanikio makubwa.

Ametoa rai ya kudumisha mshikamano ili kwenda kuwaeleza vyema wananchi na hatimaye kupewa ridhaa ya kushika dola kwa maendeleo ya wananchi na nchi.

“Ujenzi wa chama hiki ni jukumu letu wanachama wenyewe wote kutoka ndani na nje ya chama chetu. Kule diaspora nao wanauliza wanapataje hizo namba ili watuchangie,” amesema.

Kati ya michango hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alichangia Sh100 milioni, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amechangia Sh50 milioni.

Sambamba nao, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wasira amechangia Sh20 milioni, huku Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akichangia Sh20 milioni, kama alivyochangia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Kwa upande wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amechangia Sh20 milioni, Spika wa Bunge Tanzania, Dk Tulia Jackson Sh20 milioni, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Zuberi Ali Maulid Sh20 milioni.

Ukiacha vigogo, wachimbaji wadogo wa madini wamechangia Sh16.24 bilioni kati ya hizo Sh9 bilioni wameshatoa.

Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said amesema GSM imechangia Sh10 bilioni, huku Yanga ikiahidi kutoa Sh100 milioni. Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam imechangia Sh20 milioni.

Katika harambee hiyo, mawaziri na naibu mawaziri wote wa Tanzania Bara walichangia Sh365 milioni, huku upande wa Zanzibar wakichangia Sh70 milioni.