Mwanza. Zikiwa zimepita siku 55 tangu Rais Samia Suluhu Hassan azindue Daraja la JPM, maarufu kama Kigongo-Busisi, idadi ya magari kutoka ndani na nje ya nchi yanayovuka yanatajwa kuongezeka.
Rais Samia alizindua daraja hilo Juni 19, 2025 na kisha kuanza kutumika.
Kabla ya daraja hilo kuanza kutumika, wananchi walikuwa wakitumia vivuko kuvuka kati ya Kigongo Wilaya ya Misungwi na Busisi wilayani Sengerema, safari iliyochukua wastani wa dakika 40 hadi saa moja.
Hali hiyo ilisababisha ucheleweshaji wa safari na mara nyingine usumbufu kutokana na ratiba za kivuko na changamoto za hali ya hewa.
Kwa sasa, kupitia daraja hilo lenye urefu wa kilomita tatu, muda wa kuvuka umepungua hadi dakika tatu hadi tano, bila foleni jambo linalopunguza gharama na muda wa safari.
Akizungumza leo Jumanne, Agosti 12, 2025, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Ambrose Pascal, amesema wingi wa magari yanayovuka darajani hapo ni matokeo ya ujenzi wa daraja hilo.

Meneja wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza, Isaka Moga Kulwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje (wa pili kushoto) alipoutembelea leo Agosti 12, 2025.
“Matokeo tunayoyaona kwa sasa ni ongezeko la magari mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi yanayotumia barabara hii. Utaona hata barabara yetu ya kutoka Usagara kwenda mjini sasa imezidiwa na magari kwa sababu ya daraja hili kufunguliwa rasmi.
“Vilevile, idadi ya watu imeongezeka, imani yangu kuwa uchumi unakua siku hadi siku,” amesema Pascal.
Ameshauri Watanzania kutumia nafasi hiyo kuwekeza katika maeneo ya jirani na sehemu mbalimbali, hasa vijana, kwa ajili ya kujiongezea kipato na hata wenye uwezo kuwekeza kwenye biashara zitakazowaongezea kipato.
“Ninatoa pongezi kwa juhudi za Serikali ilizofanya kujenga daraja lenye urefu wa kilomita tatu, upana wa mita 28, lenye njia mbili kila upande na njia ya watembea kwa miguu. Kimsingi mambo kama haya tulikuwa tunayaona katika nchi za Ulaya,” amesema.
EAC yalifurahia daraja la JPM
Katibu Mkuu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Masinde Bwire amesema wanajivunia uwekezaji huo utakaozinufaisha nchi za Afrika Mashariki kiuchumi.
“Sisi kama Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria tunajivunia uwekezaji wa miundombinu inayosaidia nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuunganishwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara inayoshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Uganda, Edith Mwaje ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa ujenzi wa daraja hilo, akisema ni kiungo muhimu cha biashara kati ya nchi hizo.
Katika hatua nyingine, Mwaje ametembelea pia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka na kusema kuwa mradi huo ni wa kimkakati kwa maendeleo ya kikanda.
“Tunavutiwa sana na mradi huu. Una maana kubwa ikiwa utafanyika vizuri pande zote ili kuwe na usafiri wa pamoja wa bidhaa na huduma. Uganda pia tunatekeleza mradi wa SGR unaounganishwa na Mwanza hadi Dar es Salaam, ili kusafirisha mizigo na bidhaa kwa ufanisi,” amesema Mwaje.
Meneja wa mradi huo, Moga Kulwa amesema kipande hicho kina urefu wa kilomita 249 za njia kuu na kilomita 92 za njia za mpishano.
“Tumeendelea na mradi na tumefikia asilimia 64.16. Hadi sasa mkandarasi anaendelea na shughuli za ujenzi wa madaraja, vituo, na miundombinu ya umeme na mawasiliano,”amesema na kuongeza kuwa, wanategemea kukamilisha mradi huo Novemba, 2026.