Simiyu. Zaidi ya wananchi 10,000 wa kata za Malambo, Nyangokolwa, Somanda na vijiji vya jirani katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu, wameondokana na hatari ya kupoteza maisha, kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mto Ngashanda, ambalo kwa miaka mingi lilikuwa kikwazo kwa usafiri na usalama wa wananchi.
Kwa miaka mingi, mto huo ulikuwa ukiwakosesha wananchi huduma muhimu hasa nyakati za mvua, ambapo maji yalifurika na kuifanya njia hiyo kuwa hatarishi kwa matumizi ya watu wa kawaida, wanafunzi, wajawazito, wagonjwa, wazee na wafanyabiashara.
Kukamilika kwa daraja hilo lenye thamani ya Sh1.3 bilioni, kumekuwa mkombozi wa kweli kwa wananchi hao, kuhakikisha wanavuka kwa usalama, huduma za afya zinapatikana kwa urahisi, wanafunzi wanahudhuria shule kwa wakati, na biashara kustawi kwa kasi.
“Awali ilikuwa hatari kuvuka mto hasa mvua zinaponyesha, lakini sasa tuna amani. Watoto wetu wanafika shule salama, na hata sisi kinamama tunaweza kwenda kliniki bila hofu,” ni kauli ya mkazi wa Ngashanda, Editha Daud.
Daraja hilo, ambalo limekamilika kwa asilimia 100, limezinduliwa leo Jumanne, Agosti 12, 2025 na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025, Ismail Ussi, alipofanya ziara ya kukagua mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya Sh1.3 bilioni.
Ujenzi wa daraja hilo umelenga kuondoa adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwasumbua wakazi wa maeneo hayo, hususan wakati wa mvua ambapo mto huo ulikuwa ukijaa na kusababisha madhara kwa wananchi wakiwemo wanafunzi, wajawazito, wafanyabiashara na wazee.
Mkazi mwingine wa Ngashanda, Pendo Magembe amesema mto huo huwa hatari zaidi kipindi cha masika, hali inayokwamisha wananchi kufikia huduma muhimu.
“Huduma zote muhimu zipo upande wa pili wa mto, ikiwemo kituo cha afya. Nikiwa mjamzito, siku moja nilishindwa kuvuka kutokana na maji kujaa, lakini vijana walijitolea kuniokoa na kunivusha hadi nikafika salama katika Kituo cha Afya cha Muungano mjini Bariadi,” amesema Pendo.
Naye Benedictori Ngusa mkazi wa Ngashanda amesema kuwa kuna watu ambao wamepoteza maisha siku za nyuma walipojaribu kuvuka mto huo ukiwa umejaa maji.
“Huu mto ukijaa usilazimishe kupita siku za nyuma wakati daraja hili halijajengwa kuna wenzetu wamekufa hapa kwa kusombwa na maji hasa pale walipokuwa wakilazimisha kuvuka upande wa pili wakati maji yakiwa yamejaa, hivyo tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hili,” amesema.
Mwalimu Misango Suleiman wa Shule ya Msingi Ngashanda amesema ujenzi wa daraja hilo ni faraja kubwa kwao kwani wanafunzi hawatakosa tena masomo kama ilivyokuwa hapo awali pindi mvua inaponyesha.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Hussein Katakweba amesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mto Ngashanda kutarahisisha usafiri wa watu na mizigo katika maeneo ya Kata za Malambo, Nyangokolwa na Somanda, hivyo kuwaondolea wananchi adha waliokuwa wakiipata kwa miaka mingi.
“Daraja hili litawawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo yao kwa kipindi chote cha mwaka bila kukumbwa na changamoto za kuvuka mto, hasa nyakati za mvua kama ilivyokuwa hapo awali,” amesema Mhandisi Katakweba.
Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo ulianza Januari 17, 2022 na kukamilika Juni 25, 2025, ukiwahusisha makandarasi wazawa.
Ussi ameeleza kuridhishwa na ubora wa daraja na mchango wake katika ustawi wa wananchi.
“Serikali imeonyesha dhamira ya kweli ya kutatua changamoto ya usafiri. Wananchi sasa watapata huduma muhimu kwa urahisi na kuendelea na shughuli za kiuchumi bila vikwazo,” amesema Ussi.