DC Mbeya awapa majukumu bodaboda kufichua uhalifu, ukatili wa kijinsia

Mbeya. Serikali Mkoa wa Mbeya imewaonya na kuwanyooshea kidole baadhi maofisa usafirishaji (bodaboda), kutajwa kuhusika na matukio ya uharifu na ukatili katika maeneo mbalimbali jijini hapa.

Hatua hiyo imemsukuma Mkuu wa Wilaya ya Mbeya (DC), Solomon Itunda kutoa maelekezo kwa uongozi wa maofisa usafirishaji kuwa wawazi kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na matukio ya uharifu na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ili wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

Itunda  ametoa kauli hiyo leo Jumanne  Agosti 12, 2025  wakati akifungua  mafunzo ya maofisa usafirishaji, mama lishe katika Jiji la Mbeya ambayo yameratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima  (TEWW), yenye lengo la kutoa elimu ya  ujasiriamali, usalama barabarani afya na mazingira ikiwa ni kuadhimisha miaka 50.

Itunda amefungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa huku akikemea na kuonya wanaojihusisha na matukio hayo kuacha mara moja.

“Tuendelee kukabiliana na matukio ya uharifu, wapo baadhi ya maofisa usafirishaji wanabeba abiria na kuwapeleka sehemu zenye vificho na kisha kuwafanyia ukatili na uharifu,” amesema Itunda.

Amesema matukio hayo hayavumiliki, ufike wakati kuwafichua na kuwaripoti kwenye vyombo vya dora wanaobainika na siyo kuwaficha ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Katika hatua nyingine, amewataka kufanya kazi kwa malengo ili kupiga hatua za maendeleo kwa kula vizuri na kutunza familia zinazo wategemea.

“Kuna watu wanafanya shughuli za usafirishaji  wa bodaboda za mkataba usiku na mchana, lakini  hawana malengo unakuta anapata  Sh20 ,000 anahonga zote badala ya kuangalia namna bora ya malengo ya baadaye katika kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Wakati huohuo amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuunga mkono TEWW ili kubadilisha maisha ya Watanzania kwa lengo la kuhakikisha asilimia 12 za wananchi wasiojua kusoma na kuandika zinatoweka.

Kwa upande wake mkuu wa TEWW, Profesa Philipo Sanga amesema  Mkoa wa Mbeya umeshika nafasi ya tano kuondokana na changamoto  ya watu kutojua kusoma na kuandika kwa kuwa na asilimia 87.6 huku Jiji la Dar es Salaam ukiwa na asilimia 97.5.

Amesema mbali na takwimu hizo  katika halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kuna asilimia 20.2 hawajui kusoma na kuandika, sambamba na Wilaya ya Chunya  asilimia 21.1 za wasiojua kusoma na kuandika .

“Tuombe hizo wilaya mbili ziwekewe mkazo ili kuondokana na kundi la watu wasiojua kusoma  na kuandikia, lakini ujio wetu Mkoa wa Mbeya kutoa mafunzo katika makundi ya maofisa usafirishaji  na mama lishe kama sehemu ya kuelekea maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Taasisi  hii,” amesema.

Kauli uongozi bodaboda kuhusishwa na uharifu

Awali, Mwenyekiti  wa Umoja wa Bodaboda  Jiji la Mbeya, Aliko Fwanda amekiri  baadhi ya maofisa usafirishaji  kuhusisha na matukio  mbalimbali ya uharifu na ukabaji.

“Ni kweli kauli iliyosemwa na mkuu wa wilaya lipo kundi la watu wasio waaminifu wanao jihusisha na matukio ya uharifu, ubakaji na ubakaji  licha ya kuwepo kwa mikakati mbalimbali ya kukabiliana nao,” amesema.

Fwanda amesema awali walikuwa na mikakati ya viongozi  wa  bodaboda kufanya doria na kuwabaini nyakati za usiku, lakini tukiwapeleka kwenye vyombo vya dora tunakosa ushirikiano, ” amesema.

New Content Item (1)

Amemuomba Mkuu wa Wilaya  kufanya mkutano na viongozi qa bodaboda Jiji na Kanda ili kuweka  mikakati  ya pamoja  kukabiliana  na kundi  hilo ambalo  nyakati za usiku limekuwa changamoto  kwa jamii hususani  wanawake.

Mkazi wa  Kata ya Mabatini, Elizabeth John amesema madereva bodaboda  wamekuwa siyo kimbilio  nyakati za usiku kwani ni  tishio jambo ambalo ujenga hofu ya kutembea na vitu vya thamani kama pochi na simu za mkononi kwa kuhofu kukabwa na kuporwa.