Dar es Salaam. Wakati Serikali ikisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia huku ikirejea mpango wake wa asilimia 80 ya Watanzania watumie ifikapo mwaka 2034, wadau wameeleza uzuri na umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo.
Kuhifadhi mazingira, kuokoa muda, usalama wa kiafya pamoja na uhakika ni miongoni mwa faida zake, licha ya takwimu kuonesha hadi sasa Watanzania chini ya asilimia 10 ndiyo wanaotumia nishati safi ya kupikia, huku idadi kubwa ikitumia nishati isiyo safi.
Katika mjadala wa Mwananchi X Space, ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) uliofanyika jana Jumatatu, Agosti 11, 2025, ukiwa na mada inayohoji: “Nini kifanyike Watanzania watumie nishati safi kupikia ili kulinda mazingira na afya zao?” wadau hao wameshauri juu ya sera, mifumo pamoja na mikakati ili kufikia malengo hayo.
Akizungumza kwenye mjadala huo, Mtafiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Governance Links, Donald Kasongi amesema Taifa linapaswa kuweka mikakati madhubuti na mifumo thabiti ili kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema ni muhimu kuwepo kwa mnyororo kamili unaoanzia kwenye elimu kuhusu matumizi ya nishati safi, ili kuwajengea watu uelewa wa kina na kuwaonesha umuhimu wa mabadiliko hayo.
Pia, amesema ni muhimu kuhakikisha ushirikishwaji wa kila mmoja pamoja na kuangalia gharama, ili kuwawezesha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamia kwenye nishati safi.
“Wengine wakisikia gesi wanahisi ni biashara tu. Kumbe kuna nishati nyingine safi za kutumia. Lazima tuangalie maisha ya wananchi wetu, tuangalie huu mkakati wa kuelekea mwaka 2034, lazima tujiwekee malengo ili kufikia huko,” amesema.
Amesema katika kufanikisha hilo, lazima kurudi nyuma na kuangalia mfumo wa maisha ya watu, halafu waitwe wadau wa nishati, wanahabari, sekta ya nishati, biashara na fedha, pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kusaidiana katika kutoa elimu.
Mchambuzi wa takwimu na mwandishi wa habari za mazingira wa gazeti la Mwananchi, Halili Letea amesema Watanzania chini ya asilimia 10 ndiyo wanaotumia nishati safi ya kupikia, huku idadi kubwa ikitumia nishati chafu.
Amesema kuwa nishati chafu ina athari kwa mazingira, akinukuu Mpango Kabambe wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira 2022–2032 unaoonesha ekari 439,000 kila mwaka hukatwa kwa ajili ya nishati.
“Hii inasababisha uharibifu wa ikolojia na vizazi vinavyokuja kupata rasilimali hizi. Pia mpango huu unaonesha maeneo yanayokatwa misitu zaidi ni kanda ya magharibi, hususan mikoa ya Tabora.
“Kwa hiyo, nchi imekuja na mkakati huu kuokoa mazingira na kusaidia Sera ya Taifa ya Mazingira ya 2015 ambayo ililenga kuimarisha mabadiliko ya nishati, yaani watu kuachana na kuni na mkaa na kutumia nishati safi na kuwezesha majiko mazuri,” amesema.
Kulingana na mkakati huo, Halili amesema watu takribani 33,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kunakosababishwa na nishati zinazotumika.
Wakati akitaja athari hizo, Halili amesema kundi la wanawake ndiyo waathirika zaidi kwani wanahusika kwa kiwango kikubwa kwenye mapishi na matumizi ya nishati hizo, lakini pia hutafuta kuni na mkaa kila siku ili wapikie.
“Wanawake wanapoteza fursa za kiuchumi kwa kupoteza muda mwingi kutafuta kuni na mkaa badala ya kufanya shughuli nyingine, lakini pia wanaathirika zaidi kiafya na kijamii. Wanaharibu familia na mahusiano kwani analazimika kutoka mapema kutafuta nishati na kuacha familia kwa muda mrefu,” amefafanua.
Salari ametaja suala la elimu kuwa ni muhimu na kwamba elimu inabidi itolewe zaidi katika ngazi ya chini kwenye jamii, shuleni na mitaani, na hili ni rahisi zaidi kama zitashirikishwa redio za vijijini.
“Hili litawezesha wengi kufikiwa, hata wasiojua kusoma, kwani kwa mujibu wa Takwimu za Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2021, asilimia 24 ya Watanzania ni mbumbumbu,” amesema.
Meneja wa Programu wa Taasisi ya Nature and Climate Danmission East Africa, Dickson Shekivuli amesema nishati ni maisha, kwani ni vigumu kuitenganisha jamii na matumizi ya nishati.
Amesema nishati ni chanzo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya chakula na ujenzi wa miundombinu kama barabara, hususan kuchemsha lami. Hivyo, mabadiliko yanayohitajika sasa yanapaswa kwenda sambamba na ubunifu wa kiteknolojia.
Shekivuli ameongeza kuwa, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuna utashi wa kisiasa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hivyo, ni muhimu kwa wataalamu kupewa nafasi ya kubuni vyanzo vipya vya nishati vinavyofaa kwa mazingira ya Kitanzania.
“Nchini Indonesia wamebuni nishati itokanayo na taka. Ukiangalia majiji makubwa kama Dar es Salaam na Mwanza, tunazalisha taka kwa wingi na zinaweza kutumika kama chanzo cha nishati, kuwezesha jamii kuendelea kutunza mazingira,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kubuni fursa za ajira katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji na usambazaji wa nishati safi, akisema hatua hiyo itawawezesha vijana na akina mama kujipatia kipato na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nishati safi.
Shekivuli pia ameiomba Serikali kufanya mapitio ya tozo mbalimbali zinazohusu gesi na umeme, ili kupunguza gharama na kuwahamasisha wananchi wengi zaidi kuhamia kwenye matumizi ya nishati hizo kwa unafuu na urahisi.
Naye Profesa katika Ndaki ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Amos Majule, amesema nchi imeanza vizuri kwenye utekelezaji wa mkakati wa nishati safi ya kupikia, akisisitiza uwekezaji zaidi na utekelezaji wa matokeo ya tafiti zinazofanywa.
“Zipo tafiti zinazofanywa na zilizokamilika kwenye masuala haya. Hizi zifanyiwe kazi ili tuendelee kutunza mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Profesa Majule pia ameshauri elimu kutolewa shuleni kwani wanapojifunza watoto, ni rahisi wao kuelewa na kufikisha elimu hiyo kwa wazazi na walezi wao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disability, Michael Salari, amesema tafiti mbalimbali za kimataifa zinaonesha kuwa takribani asilimia 90 ya watu wenye ualbino hufariki dunia kutokana na saratani ya ngozi.
Ameeleza kuwa ukataji hovyo wa miti kwa ajili ya nishati si tu unaathiri mazingira, bali pia unawanyima watu wenye ulemavu, hususani wenye ualbino, maeneo ya kupata kivuli.
“Kundi hili limekuwa likikumbwa na changamoto kubwa kunapotokea uharibifu wa mazingira. Hapa nchini, takribani asilimia 80 ya vifo vya watu wenye ualbino vinahusishwa na uharibifu wa mazingira na matumizi ya nishati chafu,” amesema.
Salari amebainisha kuwa ukataji miti ovyo unawaweka katika hatari zaidi kutokana na athari za moja kwa moja za mionzi ya jua, ambayo ni chanzo kikuu cha saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino, kutokana na kukosa kinga ya asili ya ngozi.
Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuongeza juhudi za kusambaza nishati safi vijijini, kwani maeneo hayo hukumbwa na changamoto kubwa zaidi. Wagonjwa wengi wa saratani kutoka vijijini hufika hospitalini wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa, hali ambayo mara nyingi huchochewa na uharibifu wa mazingira.