Jaji Mkuu afungua milango maboresho ya sheria, sera

Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju ametoa wito kwa Watanzania wote kutoa maoni yao kuhusu maboresho ya sheria na sera, ili kuchochea utawala wa sheria, kukuza demokrasia na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mjadala wa kitaifa kuhusu maboresho ya sheria na sera, Jaji Masaju amesisitiza kuwa majadiliano yako wazi kwa wadau wote, lakini mabadiliko yatakayopendekezwa ni lazima yawe kwa maslahi ya umma na yaheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mjadala huo umeandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na vyama vya wanasheria, ukiwa na lengo la kujadili na kupendekeza maboresho yatakayowezesha ujenzi wa taifa lenye haki, usawa na utawala bora.

“Serikali hatujafunga mipango, leteni maboresho ya sheria, lakini pia lazima yatokane na matakwa ya wananchi sio mashinikizo kutoka nje na pia mje na hoja na sababu za kutaka maboresho hayo,” amesema Jaji Masaju.

Amesema ni muhimu wanasheria na Watanzania kutambua kuwa haiwezekani kuwa na mabadiliko kwa kuiga wengine ambao wana historia yao, mila na taratibu na kuiga kila kitu kunaweza kubomoa nchi.

Hata hivyo, Jaji Masaju amepongeza THRDC kwa kuandaa kongamano hilo ambalo linaleta majadiliano ya pamoja ya maboresho ya sheria na sera kwa kukaa mezani.

Amesema vyama vingine vya kitaaluma na mashirika wanaweza kuleta hoja na kujadiliwa kwa pamoja kwa sababu Tanzania siyo ya kundi fulani bali ni ya Watanzania wote wenye nia njema ya kuchochea ustawi wa wananchi.

Awali, mwenyekiti wa baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NaCoNGO), Mwantumu Mahiza amesema Serikali inatambua kazi nzuri za Asasi za kiraia nchini na inaendelea kuunga mkono.

Mahiza amesema changamoto zilizopo zinaendelea kufanyiwa kazi na hatua kubwa imepigwa katika kutatua changamoto za asasi za kiraia nchini tofauti na miaka ya nyuma.

Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa amesema THRDC kwa kushirikiana na vyama vya mawakili inaona kuna haja ya kuwepo maboresho ya sheria kadhaa ili kuchochea ukuaji wa demokrasia, kutominywa utendaji kazi wa asasi za kiraia, kuchochea ustawi wa wananchi na ulinzi wa haki za binaadamu.

Ole Ngurumwa amesema kuwa, kupitia tafiti na uchambuzi mbalimbali uliofanyika  ikiwemo utafiti kuhusu hali ya mfumo wa utetezi wa haki za binadamu nchini, pamoja na uchambuzi wa pengo kati ya uwezo na mahitaji ya asasi za kiraia uliofanywa na Wakili Clarence Kipobota, imebainika kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa katika eneo hilo.