Kinyozi aliyenajisi mtoto wa miaka sita, jela maisha

Arusha.”Tamaa imemponza. Ndivyo unavyoweza kusema kilichomkuta kinyozi, Nickson Nyala, ambaye Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kosa la kumnajisi mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miaka sita.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 4, 2021 katika eneo la Karifonia, mkoani Geita ambapo Nickson alipelekewa mtoto huyo ili amnyoe nywele.

Shahidi wa nne ambaye ni mama mdogo wa mwathirika wa tukio hilo, aliieleza mahakama kuwa alimpeleka mtoto huyo saluni na kwenda sokoni, ambapo aliporejea hakumkuta saluni hapo na alipofika nyumbani alimkuta mtoto huyo akilia na kueleza mrufani alimpeleka nyumbani kwake na kumnajisi.

Nickson alihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, baada ya kumkuta na hatia ya kosa hilo kinyume na kifungu cha 130 (1), (2) (e) na 131 (1) (3) ya Kanuni ya Adhabu.

Hii ni rufaa yake ya pili kukwaa kisiki ambapo awali Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, ilitupilia mbali rufaa yake.

Rufaa hiyo ya jinai namba 552/2023 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini ambao ni Augustine Mwarija, Issa Maige na Lameck Mlacha ambao walitoa hukumu hiyo jana Agosti 11, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia rekodi ya rufaa hiyo na sababu za rufaa na kujiridhisha kuwa kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka.

Siku ya tukio shahidi wa nne alimpeleka mtoto saluni baada ya kutumwa na mama wa mtoto huyo ambaye katika kesi hiyo alikuwa shahidi wa pili, ambapo alimwacha na kwenda sokoni kununua viazi.

Shahidi huyo wa pili alimkagua sehemu za siri mtoto huyo na kugundua alikuwa na michubuko, ambapo alimweleza mume wake kisha wakaripoti Kituo cha Polisi cha Katoro.

Alipewa fomu namba tatu (PF3) na mwathirika wa tukio hilo kupelekewa Kituo cha Afya Katoro ambapo alichunguzwa na shahidi wa tano, ofisa wa kliniki, Kabula Kipete ambaye alibaini mtoto huyo alikuwa na michubuko ukeni.

Shahidi wa nne akitoa ushahidi mahakamani hapo alieleza baada ya kutoka sokoni na kurejea saluni hakumkuta mwathirika wa tukio hilo wala mrufani na kuamua kumpigia simu shahidi wa pili kumuuliza kama mtoto huyo alirudi nyumbani.

Alieleza kuwa akiwa bado anapiga simu alimuona mrufani akirejea saluni huku akiwa amembeba mwathirika wa tukio hilo mabegani mwake na alipomuuliza kwa nini mtoto huyo hajanyolewa nywele, mrufani alidai mashine ya kunyoa nywele iliharibika hivyo alimpeleka nyumbani kwake.

Alieleza kuwa mwathirika wa tukio hilo alikuwa akilia lakini alipoulizwa kwa nini yuko katika hali hiyo, hakueleza sababu hiyo hadi alipofika nyumbani na kumweleza mama yake kuwa alibakwa na mrufani.

Mwathirika wa tukio hilo ambaye alikuwa shahidi wa kwanza, alieleza baada ya shahidi wa nne kumuacha saluni, mrufani alimpeleka nyumbani kwake, kisha akamlaza kitandani, akavua nguo zake na kumnajisi.

Alieleza kuwa alipata maumivu kutokana na kitendo cha mrufani na kuwa alimrudisha saluni huku akilia na hakumweleza mama yake mdogo kwa nini alikuwa akilia, hadi alipofika nyumbani na kumweleza mama yake.

Jirani wa mrufani katika Mtaa wa Karifonia, Ruchius Tibendagita (shahidi wa tatu), alithibitisha kuwa alishuhudia mrufani na mwathirika wakiingia na kutoka katika makazi ya mrufani.

Alieleza kuwa wakati mwathirika akitoka nyumbani kwa mrufani, alikuwa akilia na alipomuuliza mrufani kwa nini mtoto huyo alikuwa akilia, alimjibu alikuwa anataka fedha kwa ajili ya kununua ‘ice cream’ lakini hakuwa na pesa.

Katika utetezi wake mrufani alieleza siku ya tukio akiwa kazini kwake walienda watu wawili ambapo aliachiwa mtoto huyo kwa ajili ya kumnyoa na mama mdogo wa mtoto huyo aliporudi na kukuta mtoto hajahudumiwa, alimlalamikia na kumchukua mtoto.

Alieleza kuwa mama mdogo huyo alienda kulalamika kwa balozi ambapo mrufani aliitwa na kuelezwa kuwa analalamikiwa kwa kosa la kumpiga mtoto huyo, lakini  aliporejea kazini kwake alikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Katoro na kufikishwa mahakamani.

Mrufani huyo alikiri kujulikana na mwathirika wa tukio hilo kwani alikuwa akipelekwa saluni kwake mara kwa mara na kukiri alimfahamu mama yake kwani kabla tukio alikuwa na ugomvi naye.

Mahakama hiyo ya chini baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ilijiridhisha kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka ambapo hakimu aliegemea ushahidi wa shahidi wa kwanza, tatu, tano na wa pili.

Kuhusu  suala la utambulisho, Mahakama ya mwanzo iliona kwamba mrufani alikuwa anajulikana sana na mwathirika wa tukio.

Katika rufaa ya kwanza Jaji aliidhinisha hukumu dhidi ya mrufani na kuunga mkono matokeo ya mahakama ya chini kwamba, ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa wa kutosha na hivyo kuthibitisha bila shaka kosa aliloshtakiwa.

Katika rufaa ya pili, mrufani huyo alikuwa na sababu nne za rufaa ambazo ni Jaji alikosea kisheria kushikilia hukumu ya mrufani ambayo ilitokana na shtaka lenye dosari, hukumu ilitokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha na kesi dhidi yake haikuthibitishwa.

Rufaa hiyo mrufani hakuwa na uwakilishi wa wakili huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Luciana Shabani.

Wakili Luciana alieleza kuwa hukumu ya Mahakama ya mwanzo ilizingatia masharti ya kifungu cha 312 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai,  akitoa mfano wa kesi ya Emmanuel Phabian dhidi ya Jamhuri (Rufaa ya Jinai namba 259/2017), kuunga mkono hoja yake.

Wakili huyo alieleza baada ya kifungu ambacho mshtakiwa alishitakiwa chini yake kimeelezwa katika hukumu, maelezo kwamba mshtakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshitakiwa.

Kuhusu shtaka kuwa na dosari wakili huyo alieleza kuwa  maneno yaliyoandikwa kwa mkono kwenye karatasi ya shtaka ya kusahihisha jina la mshtakiwa (mrufani), hayakufanya shtaka kuwa na dosari.

Alieleza baada ya mabadiliko hayo yalionyesha jina sahihi la mshtakiwa na mrufani hakupinga jina lake wakati wa usikilizwaji wa awali na kuwa shauri hilo lilithibitishwa bila kuacha shaka.

Baada ya kupitia mwenendo na kusikiliza hoja za pande zote mbili majaji hao walichambua sababu za rufaa na kueleza kuhusu kufutwa jina la Baraka Seif na kubadilishwa na kuandikwa jina la mrufani hakujafanya shtaka kuwa na dosari, masahihisho yaliyofanyika Agosti 13, 2021 na mrufani kusomewa na kukiri jina lake.

“Pia, tunakubaliana na Wakili wa Serikali kwamba, kushindwa kueleza muda ambao kosa lilifanyika hakukufanya mabadiliko hayo kuwa na dosari,” amesema

 Kuhusu sababu ya kuwa kesi haikuthibitishwa bila shaka yoyote Jaji Mwarija amesema kutokana na ushahidi uliopo kwenye rekodi, wanakubaliana na Wakili wa Serikali Mwandamizi kuwa kesi hiyo ilithibitishwa bila shaka yoyote.

 “Kuanza na umri wa mwathiriwa, kama ilivyoelezwa na Bi Shabani, hiyo ilithibitishwa na mama yake (shahidi wa pili), alikuwa mtu sahihi kufanya hivyo kama ilivyoshikiliwa miongoni mwa wengine, ”

Jaji Mwarija amesema ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo uliungwa mkono na shahidi wa tano ambaye alithibitisha kuona michubuko kwenye sehemu za siri za mtoto huyo, na kuwa ni kanuni hilo kufanyika kwamba ushahidi wa mwathirika wa tukio katika kosa la ngono.

“Kuhusu utambulisho wa mrufani, ambao ni msingi wa sababu ya tatu ya kukata rufaa, pia tunakubaliana kwa heshima na Wakili wa Serikali Mwandamizi kwamba mrufani alitambuliwa ipasavyo,”amesema Jaji.

Majaji hao walihitimisha kuwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka uliaminiwa na Mahakama mbili za chini na kuwa hawaoni uhalali wowote katika sababu za rufaa, na kuitupilia mbali.