Maema atupia moja Afrika Kusini ikiichapa Guinea CHAN 2024

Kiungo mshambuliaji wa Afrika Kusini, Neo Maema amefanikiwa kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea.

Katika mchezo huo wa kundi C uliochezwa leo Agosti 11 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Kampala, Uganda imeshuhudiwa Maema akiiandikia bao la kwanza Afrika Kusini katika dakika ya 10.

Maema ambaye anatajwa kujiunga na Simba dilisha hili la usajili akitokea Mamelodi Sundowns, bao lake halikuweza kudumu kwani katika dakika ya 37 mshambuliaji wa Guinea, Moussa Camara alifunga bao la kusawazisha na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikitoshana nguvu.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Afrika Kusini ilirejea kwenye uongozi, safari hii akifunga Thabiso Kutumela mshambuliaji anayekipiga kwenye Klabu ya Richards Bay.
Hadi dakika 90 za mwamuzi zinamalizika Afrika Kusini iliibuka na ushindi wa kwanza ikifikisha jumla ya pointi nne katika nafasi ya pili sawa na vinara wa kundi hilo Algeria ambao wanaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga.

Mchezo mwingine wa kundi C utawakutanisha wenyeji Uganda dhidi ya Niger. Katika mchezo huu Uganda inahitaji kupata pointi tatu ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali kwani katika mechi mbili ilizocheza imepoteza moja na kushinda mara moja ikiwa katika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa Niger nao bado wana nafasi ya kufuzu robo fainali. Licha ya kubuluza mkia kwenye kundi, Niger imeshacheza mechi moja ambayo ilipoteza dhidi ya Guinea.

Iwapo timu hiyo ikipata ushindi kwenye mchezo wa leo itafufua matumaini ya kusaka ushindi mwingine kwenye mechi mbili itakazokuwa imebakiza dhidi ya Algeria na Afrika Kusini.

Hata hivyo, Uganda bado inapewa nafasi ya kufanya vizuri zaidi kutokana na nguvu kubwa ya mashabiki pamoja na kiwango ilichoonesha kwenye mechi dhidi ya Guinea ilipoichapa mabao 3-0.