KOCHA wa Kenya, Benni McCarthy amesema ushindi wao wa kihistoria dhidi ya Morocco kwenye CHAN 2024 umetokana na mbinu alizojifunza kutoka kwa Jose Mourinho, akisisitiza kucheza pungufu ya mchezaji mmoja si kisingizio cha kupoteza kama timu ina nidhamu na mipango sahihi.
Ushindi wa Kenya dhidi ya Morocco, uliifanya timu hiyo kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa kundi A huku ikiwa na pointi saba.
McCarthy alisema, “Nilicheza chini ya kocha mmoja Jose Mourinho mtaalamu wa kusimamia mechi ngumu. Tulizoea kumaliza michezo tukiwa na wachezaji pungufu, na bado tukapata ushindi. Nilijifunza kwake wapi pa kufunga mianya na ni nani wa kumtoa ili timu ibaki imara.”
Kauli hiyo ilikuja baada ya Kenya kuwachapa mabingwa mara mbili wa CHAN, Morocco, kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Moi, Kasarani, licha ya kucheza kipindi cha pili wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja.
Bao pekee katika mechi hiyo lilipatikana dakika ya 42 kupitia Ryan Ogam hata hivyo, dakika mbili baadaye, kiungo Chrispine Erambo alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Anas El Mahraoui.
McCarthy alisema alitumia moja kwa moja falsafa ya Mourinho kwa kupunguza mashambulizi ya mbele, kubakiza mchezaji mmoja “mwenye pumzi” kusumbua safu ya ulinzi ya mpinzani, na kisha “kupaki basi” mbele ya lango.
Wakati akicheza soka la kulipwa, McCarthy aliwahi kunolewa na Mourinho, FC Porto ya Ureno na kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2003–04.