Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetaja mikoa sita itakayoshuhudia vipindi vya mvua na ngurumo za radi kwa siku 10.
Hali hiyo iliyoanza kushuhudiwa kuanzia jana Agosti 11, 2025, itadumu hadi Agosti 20, 2025. Mikoa inayotarajiwa kukumbana na hali hiyo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara.
Kuhusu hali ya ukavu, Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki yenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro itakuwa na hali ya ukavu.
“Pwani ya Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam, na visiwa vya Unguja na Pemba itakuwa na mvua nyepesi maeneo machache,” imeeleza taarifa hiyo ya TMA.
Kwa maeneo ya Magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora nako kunatarajiwa hali ya ukavu.
Vilevile, kanda ya kati ya mikoa ya Dodoma na Singida nako hali ya ukavu inatarajiwa.
“Nyanda za Juu Kusini Magharibi, yaani Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa, kutakuwa na hali ya ukavu,” taarifa hiyo imeeleza.
Maeneo ya Pwani ya Kusini, hasa mikoa ya Mtwara na Lindi, matarajio ni hali ya ukavu, huku ukanda wa kusini, yaani Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro, hali ya ukavu pia inatarajiwa.