‘Msafara wa Chaumma usipime, wateka vijana’

Dodoma. Matarumbeta, ngoma za asili na kelele za muziki vilitawala mitaa ya Njedengwa leo, wakati mgombea urais kupitia Chaumma, Salum Mwalimu, alipowasili kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Eneo la Njedengwa, lilio umbali wa takriban kilomita 4.8 kutoka katikati ya jiji la Dodoma, ndiko yalipo makao makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Salum Mwalimu akiwa na mgombea mwenza wake, Devotha Minja, waliwasili kwa msafara mkubwa uliovutia macho ya wengi ukiwa na magari, pikipiki, vikundi vya ngoma, matarumbeta na vijana waliokuwa na hamasa kubwa na ‘mzuka’ wa aina yake.

Dalili za Chaumma kuandaa mapokezi ya nguvu zilianza kuonekana mapema, ambapo waandishi wa habari walipatiwa vitambulisho maalumu, sawa na vile vilivyotolewa wakati Rais Samia Suluhu Hassan wa CCM alipokwenda kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo pia.

Mbali na dalili hizo za maandalizi makubwa, ulinzi uliimarishwa katika eneo la jengo la INEC, ambalo liko pembezoni na limezungukwa na milima ya mawe.

Mnamo saa 5:57 asubuhi, msafara mrefu ulioongozwa na gari la wazi la Polisi waliovaa sare rasmi uliwasili eneo hilo. Msafara huo ulifuatiwa na pikipiki kati ya 120 hadi 150, zote zikiwa zimepambwa kwa bendera za Chama cha  Ukombozi wa Umma.

Mgombea urais kwa tiketi ya Chaumma, Salum Mwalimu, alionekana akiwa amesimama juu ya gari jeupe la wazi, akipungia wananchi mikono.

Mgombea mwenza wake, Devotha Minja, pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe nao walikuwa kwenye magari tofauti ya rangi nyeusi, wakiwa wamesimama na kuwapungia wafuasi wao mikono.

Hata hivyo, ilichukua zaidi ya dakika 15 kwa wagombea hao kushuka kwenye magari yao na kuingia ndani ya ukumbi, kipindi ambacho wapambe wao waliendelea kucheza muziki na kushangilia kwa furaha.

Dakika tisa baadaye, Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila, aliwasili akifuatana na wabunge wa zamani wa viti maalumu, Catherine Ruge na Suzan Kiwanga.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Jacobs Mwambegele (kulia) akimkabidhi fomu ya uteuzi wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgombea wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, katika ofisi za tume hiyo, Njedengwa jijini Dodoma leo Agosti 12, 2025.

Walielekea moja kwa moja kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima kisha wakatoka naye kwenda kuwapokea rasmi wagombea.

Idadi ya watu waliopewa ruhusa ya kuingia katika viwanja vya INEC ilikuwa kubwa, na ilizidi ile ya vyama vingine ukiondoa CCM.

Baada ya kukabidhiwa fomu za kugombea urais, Mwalimu, alizungumza na waandishi wa habari, akieleza sababu anazoamini zitamfikisha kwenye ushindi katika uchaguzi ujao.

“Sina deni na mtu. Mimi ni msafi; sijawahi kumbeba mtu wala kumuingiza sehemu yoyote kwa kutumia kimemo. Hata mgombea mwenza wangu ni msafi, na rekodi zake mnazifahamu vizuri,” amesema Mwalimu kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa wakati wa mabadiliko umefika, kwani wanatoka katika chama kinachojali watu na chenye misingi ya uadilifu, hivyo hawana sababu ya kuwa na woga au hofu katika kufanya maamuzi makubwa kwa ajili ya nchi.

Katika hotuba yake, Mwalimu amesisitiza kuwa jambo la kwanza atakalolifanya pindi atakapoingia Ikulu ni kuhakikisha upatikanaji wa Katiba Mpya itakayopitia upya sheria mbalimbali za nchi ambazo kwa sasa hazina tija kwa wananchi.

Msafara wake uliondoka katika ofisi za INEC saa 6:43 mchana kwa mbwembwe zilezile kama alipoingia, huku ikionekana wazi kuwa sehemu kubwa ya magari ya msafara huo yaliendeshwa na wanawake ishara ya ushiriki mpana wa kijinsia katika harakati za kisiasa za chama hicho.