Mwendokasi Mbagala kumekucha, vituo vyaanza kusafishwa

Dar es Salaam. Maandalizi ya kuanza kwa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili, katika barabara ya Mbagala (Kilwa), sasa yameanza kuchangamka.

Hii ni baada ya kupita wiki moja tangu mabasi 99 kati ya 250 yatakayotumika katika awamu ya kwanza kutoa huduma, kuingia jijini Dar es Salaam yakitokea nchini China yalikotengenezwa.

Mabasi hayo, mali ya Kampuni ya Mofat, ni sehemu ya mabasi 250 yatakayotoa huduma katika njia hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.

Barabara ya Mbagala yenye urefu wa kilomita 20.3 kutoka Mbagala hadi Gerezani, ilijengwa na Kampuni ya Sinohydro kutoka China na ilikabidhiwa kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) tangu Agosti 2023.

Katika awamu hiyo, kampuni hiyo ndiyo imepewa mkataba wa miaka 12 kutoa huduma hiyo na mabasi yake yatatumia nishati ya gesi asilia barabara hiyo inayohitaji jumla ya mabasi 755.

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia aliimbia Mwananchi kuwa malengo ya mabasi hayo kuanza kutoa huduma ni ndani ya mwezi huu ( Agosti), kutokana na wananchi kusubiria kwa muda mrefu.

Dk Kihamia amesema licha ya ujenzi wa mageti janja kutokamilika kujengwa ambayo abiria wangeyatumia kupita kwa kutumia kadi, wameona waanze na tiketi kwa ajili ya kipindi cha mpito.

Pia, taarifa kutoka chanzo cha kuaminika, inaeleza kuwa, malengo ni kuanza kuwaingiza madereva barabarani wiki hii kama moja ya kufanya majaribio na kuizoea njia hiyo na tayari madereva 150 wamekidhi vigezo na kupitishwa kuifanya kazi hiyo.

Hata hivyo, wakati mabasi hayo yakiwa bado yamehifadhiwa Bandari ya Dar es Saalam hadi sasa, usafi umeanza kufanyika kwa kasi katika vituo.

Leo Jumanne Agosti 12, 2025, Mwananchi imepita katika vituo hivyo na kushuhudia usafi ukifanyika kuanzia maeneo ya Kurasini Ufundi hadi Mbagala kukiwa na watu wanafanya usafi wakiwa na mafagio na majaba ya maji.

Wapo walioonekana wakiwa wanafuta vioo, pia, wapo walioonekana wakipiga deki na kumwaga maji ndani ya vituo hivyo.

Vilevile, vituo vyote vilionekana mageti yake kufunguliwa, mengine yakifunguliwa upande mmoja na mengine pande zote na kuwepo kwa mifuko mikubwa myeusi pembezoni mwa vituo hiyo iliyotumika kuwekea takataka.

Wakizungumza kwa masharti ya kutaotajwa majina, baadhi ya wafanya usafi wamesema usafi huo wameuanza leo na ni kazi ya kusafisha vituo vyote vilivyopo katika barabara hiyo.

“Kama unavyoona, tunafanya usafi kwa kuwa ukweli ni kwamba vituo vilikuwa vichafu, hata kwa nje mkipita mlikuwa mnaviona, isingekuwa rahisi watu kuanza kuvitumia bila usafi,” amesema msafishaji huyo.

Ukiacha suala la usafi, pia, vizuizi vyote vilivyokuwa vimewekwa katika barabara hiyo vimeondolewa, jambo ambalo limesaidia kupunguza foleni kwa kuwa sasa magari madogo, bodaboda, bajaji na maguta yanapita katika barabara hiyo huku malori na daladala yakiendelea kutumia njia ya kawaida.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Baadhi ya madereva wanaotumia barabara hiyo wamesema hilo limetokea tangu Jumamosi na kueleza kuwa imewasidia kuepuka foleni iliyokuwa ni kero katika barabara hiyo tangu ilipopigwa  marufuku barabara hiyo kutumika.

Vilevile, Mwananchi imeshuhudia baadhi ya maofisa wanaosemekana ni kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wa Dart, wawakilishi kutoka Kampuni Sinohydro iliyotengeneza miundombinu wakiwa wanafanya kaguzi katika maeneo mbalimbali.

Walionekana katika mataa ya Kamata, na  wiki iliyopita Mwananchi iliripoti kuwepo kwa kipande cha barabara ambacho hakijamalizika kutengenezwa.

Pia, wengine walikuwepio ndani kituo kikubwa cha mabasi hayo Mbagala Rangi tatu ambako mabasi hayo yataanzia safari zake na kupatumia pia kama karakana na sehemu ya kujazi gesi.

Aidha, katika Kituo cha Africab Mivinjeni, eneo ambalo mwandishi wa habari hizi wiki iliyopita alishuhudia nguzo mbili za taa za kuongozea magari zilikuwa zimedondoka maeneo hayo baada ya kugongwa na gari, tayari zimeondolewa.

Wakitoa maoni yao katika hilo, baadhi ya wananchi akiwamo Dyana George, mkazi wa Mtoni, amesema sasa wanaona kweli mambo yanaenda kuanza.

“Kama na usafi wameanza kuufanya, kweli mambo yameiva kwa kuwa tuna imani hawawezi tena kupaacha pachafuke ndio waweke mabasi barabarani,” amesema Dyana.

Meshack Lucas, mkazi wa Kijichi amesema pamoja na hilo lililofanyika, bado haamini mpaka pale atakapoona mabasi hayo barabarani na yakiwa yameanza kutoa huduma kwa abiria.