Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Pili Mnyemaakizungumza.
Na Khadija Kalili – Michuzi TV
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, leo ameanza rasmi ziara yake ya kikazi kwa kutembelea Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha. Katika ziara hiyo, amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akitoa wito kwa viongozi na watendaji kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa manufaa ya Mkoa.
“Naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kubuni vyanzo vipya vya mapato. Hili ni miongoni mwa maagizo niliyopatiwa,” alisema Mnyema, akionesha dhamira ya kuimarisha mapato ya Halmashauri na Mkoa kwa ujumla.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa mafanikio katika usimamizi wa miradi yenye tija, na kusisitiza nidhamu, uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Katika ziara hiyo, Mnyema alitembelea miradi ikiwemo ujenzi wa Shule ya Mchepuo wa Kiingereza – Mwalimu Nyerere, pamoja na mradi wa Kibaha Shopping Mall.
Ziara itaendelea kesho katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, ambapo Katibu Tawala atakutana na watumishi pamoja na kukagua miradi mingine ya maendeleo.