TOFAUTI na makundi mengine yenye timu tano, hesabu za kundi D katika michuano ya CHAN 2024 zinaonekana kuwa ngumu zaidi kutokana na idadi ya timu ambazo leo Jumanne zitacheza mechi ya pili kila mmoja kusaka nafasi ya kutinga robo fainali.
Kundi D linaongozwa na Senegal iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria, huku Congo na Sudan zikishika nafasi ya pili na tatu kila mmoja akiwa na pointi moja, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Hesabu kwa wababe hao zinaendelea tena leo kwenye Uwanja wa Amaan huko Zanzibar ambapo Senegal itakuwa ikisaka ushindi wake wa pili mfululizo kwenye kundi hilo dhidi ya Congo.
Kwa mujibu wa takwimu, Senegal imeshinda mechi tatu kati ya nne zilizopita dhidi ya Congo huku moja wakitoka suluhu, mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa katika mechi ya kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia Septemba 14, 2021 na Senegal iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Baada ya mechi hiyo ya mapema, ambayo itachezwa saa 11:00 jioni, Sudan ya nyota zamani wa timu ya taifa la Ghana, James Kwesi Appiah itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi wake wa kwanza mbele ya Nigeria ambayo ilipoteza mbele ya Senegal.
Sudan itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza katika mechi mbili za mwisho dhidi ya Nigeria kwa mabao 3-1 na 1-0 katika mashindano ya Afcon 2022 na 2018.
Mechi hizo mbili zinaonekana kuwa za mtego kwa timu zote nne kwani zinaweza kutoa mwelekeo mpya wa kundi hilo kabla ya mechi za mwisho ambazo zitaamua nani atarudi nyumbanni au kuendelea na mashindano.
Akizungumzia kuanza vibaya kwenye mashindano na hesabu za kukabiliana na Sudan, kocha wa Nigeria, Eric Chelle alisema: “Hakika hatukuanza vizuri kama tulivyotegemea, lakini bado hatujakubali hali hiyo itutumize.”
Kocha huyo aliongeza: “Tunajua changamoto zilizopo, lakini tupo hapa kupambana na kuhakikisha tunarejea katika njia sahihi.”
Kwa upande wake James Kwesi Appiah akinukuliwa na vyombo vya habari Sudan alisema: “Tunajua Nigeria ni timu yenye nguvu na uzoefu, lakini sisi pia tuko na mchezaji wenye vipaji na tupo tayari kuonyesha ubora wetu.”