Senegal yakomaa kileleni kundi D

MABINGWA watetezi, Senegal wameendelea kuongoza kundi D la mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024), licha ya kutoka sare ya bao 1-1 na Congo katika mechi ya pili  uliopigwa leo, Agosti 12, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar. 

Sare hiyo imeipa pointi moja na kuimarisha nafasi yake ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya nane.

Congo ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 19, baada ya mshambuliaji Dechan Moussavou kumalizia pasi ya Atipo.

Senegal ilijitahidi kusawazisha kipindi cha kwanza kwa kushambulia mara kwa mara, lakini ilikumbana na ukuta mgumu wa Congo.Kipindi cha pili kilianza kwa mabadiliko makubwa upande wa Senegal, ambapo kocha aliingiza wachezaji wapya akiwemo Vieux Cisse, Ousseynou Seck na Fonseca. 

Lengo lilikuwa kuongeza kasi na ubunifu katika safu ya ushambuliaji, jambo lililoongeza presha kwa Congo.

Jitihada hizo zililipa dakika ya 82 baada ya Seck kutoa pasi  iliyomkuta Samb  ambaye alimalizia na kuisawazishia Senegal.

Kwa matokeo haya, Senegal inafikisha pointi nne na kuendelea kushika nafasi ya kwanza kwenye Kundi D ikifuatiwa na Sudan yenye pointi moja  ambayo itashuka dimbani isiku kumenyana na Nigeria.

Congo inasalia na pointi moja pekee na itakamilisha mechi zake za makundi dhidi ya Nigeria.