Dodoma. Serikali imesema kuwa inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za Taifa katika sekta mbalimbali za elimu na ujuzi, afya, ajira na uwezeshaji kiuchumi na katika sekta ya teknolojia na ubunifu.
Aidha kulingana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa vijana ndiyo kundi kubwa hapa nchini kwani asilimia 34.4 ya idadi ya watu ni vijana wapatao 20,612,566 ya idadi ya wananchi wa Tanzania.
Katika kuliona hilo Serikali imefanya maboresho ya sera mbalimbali kama vile sera ya taifa ya maendeleo ya vijana, sera ya ajira na nyinginezo na mikakati inayolenga kukuza ujuzi wa vijana, kuongeza fursa za ajira na kuendeleza ubunifu utakaowawezesha kuhimili ushindani katika soko la ajira.
Akizungumza leo Jumanne Agosti 12, 2025 kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani lililofanyika jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Zuhura Yunus amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya elimu kwa kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora, jumuishi na inayojibu mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
”Kipaumbele kimeendelea kutolewa kwa elimu ya msingi, sekondari, elimu ya juu na mafunzo ya ufundi stadi, ili kuwaandaa vijana kwa maarifa na stadi zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa na kwa vijana waliopo nje ya shule, Serikali inaendelea kuwapatia ujuzi katika fani mbalimbali kupitia programu ya Ukuzaji ujuzi inayotolewa kupitia Vyuo vya Veta nchini kwa ufadhili wa Serikali na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,” amesema Yunus.

Yunus amesema afya ya vijana katika kulinda tija ya nguvu kazi ya vijana, Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya kwa vijana, ikiwa ni pamoja na huduma rafiki za afya ya uzazi, lishe, afya ya akili na kinga dhidi ya magonjwa kwa sababu vijana wenye afya bora ni msingi wa uchumi imara na jamii yenye ustawi.
Pia, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji mali, sambamba na kuchochea fursa za ajira kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi kama vile Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) na asilimia 10 zinazotengwa na Serikali za Mitaa.
”Vijana wameendelea kunufaika na mikopo ya masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali ili kuendesha shughuli zao kwa tija,” amesema.
Kwa upande wa teknolojia na ubunifu vijana wameendelea kuhamasishwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kama nyenzo ya kujifunza, kujiajiri, kubuni, na kushiriki katika uchumi wa kisasa.
Amesema suala hili limeainishwa na kuwekewa msisitizo katika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 (Toleo la mwaka 2024) katika kukuza uvumbuzi na ubunifu kwa vijana ili kuibua na kuendeleza vipaji ambapo Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya Tehama na kuhimiza uanzishaji wa vituo vya ubunifu ili kukuza vipaji vya vijana na kuunga mkono mapinduzi ya kidijitali.
Mkurugenzi wa vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Suleiman Mvunye ametoa rai kwa vijana wote nchini kushiriki katika mchakato wote wa uchaguzi kwa amani na utulivu.
”Vijana mnatakiwa kuwa makini katika kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani. Serikali inatambua kuwa hakuna maendeleo ya kweli bila vijana kushirikishwa. Ushiriki wenu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia utekelezaji wa Sera na Mikakati ya Maendeleo ni sharti la mafanikio ya Taifa letu. Mchango wenu katika jamii ni kiashiria cha kuonesha kwamba Tanzania ya leo na kesho inajengwa kwa juhudi za vijana wake,” amesema Mvunye.
”Ninatoa wito kwa vijana wote nchini kutumia maarifa, ujuzi na fursa zilizopo kwa bidii na nidhamu ili kujiletea Maendeleo yao binafsi na kusaidia katika ustawi wa Taifa letu. Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na vijana, kuhakikisha kuwa ndoto zao zinatimia,” amesema.
Mwakilishi wa vijana kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Joseph Manirakiza amesema shirika hilo limewezesha vikundi vya vijana zaidi ya 60 wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za uchumi zenye thamani ya Sh5 bilioni na kutengeneza ajira 5,000 mpaka sasa.