Dar es Salaam. Mamia ya makada, wafuasi na mashabiki wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamejitokeza katika ukumbi wa Mlimani City, inakofanyika harambee ya kuchangia kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Kati ya makada, wafuasi na washabiki hao, wapo pia wafanyabiashara mashuhuri nchini, wote wakiwa mguu sawa kushiriki harambee hiyo inayolenga kukusanya Sh100 bilioni kwa ajili ya kampeni hizo.
Taarifa kuhusu harambee hiyo, ilitangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi jana Jumatatu, Agosti 11, 2025 akiweka wazi kuwa michango hiyo itathibitisha nguvu ya wanachama wa chama hicho kwa chama chao.
Katika viunga vya Mlimani City usiku huu wa leo Jumanne, Agosti 12, 2025 kumeghubikwa na rangi za kijani na njano ambazo ndizo utambulisho wa chama hicho tawala.
Ingawa kinachofanyika ni harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya kampeni, misosi, vinywaji na burudani mbalimbali zimesheheni.
Ukiacha wale waliovalia sare za CCM zenye rangi ya kijani na njano, walikuwepo wageni waliovalia suti na mavazi mengine rasmi na yenye heshima.
Isingekuwa rahisi kutathmini uchumi wa kila mhudhuriaji kwa kuangalia aina ya mavazi waliyovaa, kwani kila mmoja amevunja kabati kadri alivyoweza kiasi cha kuonekana wote wana mizania sawia ya ukwasi.
Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan amewasili ukumbini hapo saa 2:00 usiku, akitanguliwa na wajumbe wa sekretarieti ya chama hicho, akiwemo Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi.
Viongozi wote wa kitaifa wa CCM, kutoka Bara na Zanzibar wapo ukumbini hapo, kadhalika viongozi wengine wa kiserikali na taasisi binafsi walikuwa sehemu ya wahudhuriaji.
Kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28 na Oktoba 29, 2025 siku ya Jumatano ndio upigaji kura.
Endelea kufuatilia Mwananchi