Wachezaji wapya wa Simba, Mohamed Bajaber na Jonathan Sowah wameanza kuonyesha makali yao baada ya kutikisa nyavu katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana dhidi ya Kahraba Ismailia.
Katika mechi hiyo ya maandalizi ya msimu ujao wa 2025/2026 Simba iliandika bao la kwanza lililofungwa na Mohamed Bajaber katika kipindi cha kwanza.
Bao la pili lilipatikana kipindi cha pili safari hii mfungaji akiwa ni Jonathan Sowah ambaye alimalizia vizuri pasi ya Jean Ahoua.
Baada ya mechi kumalizika Sowah ameonyesha matumaini ya kuanza kuzoeana na wachezaji wengine uwanjani.

“Nikielezea bao nililofunga nampa sifa zote Ahoua kwa kuniona na kunipasia, nadhani tumeanza kuzoeana na kuingia kwenye mfumo wa mwalimu,” amesema Sowah.
Naye kocha mkuu Fadlu Davids amesema kuwa timu ipo kwenye maandalizi mazuri na ameonyesha imani kwa wachezaji wapya kuanza kuingia kwenye mfumo mapema.
“Tumepata mchezo mzuri wenye ushindani kutoka kwenye timu yenye ushindani, katika maandalizi ya msimu uliopita ukilinganisha na sasa nadhani tumepiga hatua zaidi.
“Kipindi cha kwanza ni wachezaji watatu wa msimu uliopita ndiyo walioanza, wameweza kutekeleza na kufuata maelekezo ya mfumo wetu, Tumecheza vizuri kwa nguvu na umakini.
“Tungeweza kumaliza mchezo kwa ushindi wa mabao manne au zaidi lakini wapinzani wetu wamejilinda vema na sisi tukiwa makini tukimaliza bila kuruhusu bao,” amesema Fadlu.

Fadlu ameongeza kuwa benchi lake la ufundi litafanya mabadiliko kadhaa kuelekea kwenye mchezo mwingine wa kirafiki.
“Tutajaribu kubadilisha masuala kadhaa na mipango wa wiki mpya imeshaandaliwa na mazoezi yataongezeka ili kuandaa timu kwa mchezo ujao siku ya Jumapili,” amesema Fadlu.