Sudan yaidhalilisha Nigeria, yaing’oa mapema CHAN 2024

NIGERIA imekuwa timu ya kwanza kuaga fainali za CHAN 2024 baada ya usiku huu kufumuliwa mabao 4-0 na Sudan kwenye mechi ya Kundi D uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, visiwani Zanzibar.

Matokeo haya yameiondoa rasmi Nigeria katika mashindano baada ya kucheza mechi mbili bila kupata pointi.

Mechi ilianza kwa kasi, huku dakika ya 22 bao la Anthony Ijoma . likikataliwa kwa madai ya kuotea baada ya ukaguzi wa VAR. 

Sudan ilipata bao lao la kwanza dakika ya 25 baada ya beki wa Nigeria, Leonard Ngenge kujifunga. Dakika ya 44, Walieldin Khidir aliiongezea Sudan bao la pili kupitia mkwaju wa penalti baada ya Ngenge kufanya madhambi kuonyesha alikuwa na siku mbaya kazini na kufanya timu hiyo kwenda mapumzikoni ikiwa le 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Nigeria kufanya mabadiliko matatu ya haraka, lakini bado hawakuweza kuzima mashambulizi ya Sudan. Dakika ya 55, Tabanja aliipatia Sudan bao la tatu muda mfupi baadaye, dakika ya 62 kabla ya kuongeza jingine, likiwa la pili na kuhitimisha ushindi mnono wa mabao 4-0.

Nigeria, inayojulikana kama “Super Eagles”, ilionekana kupoteza mwelekeo na kupungukiwa na ubunifu, huku Sudan wakitumia vizuri kila nafasi waliyoipata.

Kwa ushindi huo, Sudan inafikisha  pointi nne na kuishusha Senegal kileleni kutokana na mtaji mkubwa wa mabao wakiwa na pointi sawa, Congo ipo nafasi ya tatu na pointi mbili na Nigeria ndio inaburuza mkia.

Hata kama Nigeria itashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Congo haitaweza kufikia pointi za Sudan na Senegal na kuifanya iwe timu ya kwanza kuaga michuano hiyo.