Wahamiaji haramu 39 wakamatwa Geita, wakiwamo watoto 12

Geita. Idara ya Uhamiaji mkoani Geita imewakamata wahamiaji haramu 39 raia wa Burundi, wakiwemo watoto 12, waliobainika kuingia nchini kinyume cha sheria.

Kukamatwa kwa wahamiaji hao kumetokana na operesheni maalumu inayoendelea mkoani humo tangu Julai 2025, ambapo hadi sasa zaidi ya wahamiaji haramu 300 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Geita, Donald Lyimo amesema wahamiaji hao walikamatwa katika maeneo ya Pori la Akiba Nshinde, eneo la Igate, na kituo kikuu cha mabasi Geita.

“Katika kundi hilo, wamo pia raia wawili wa Tanzania; mmoja akituhumiwa kwa kuwapangisha wahamiaji hao nyumba ya kuishi, na mwingine kwa kuwatumikisha katika mashamba ya mihogo na mahindi bila vibali,” amesema Lyimo.

Ameongeza kuwa operesheni hiyo ni sehemu ya kampeni inayoendelea kwa jina la “Mjue Jirani Yako”, ambayo inalenga kubaini, kudhibiti na kuondoa wahamiaji haramu wanaoingia na kuishi nchini kinyume cha sheria, hususan maeneo ya mipakani na mikoa yenye shughuli nyingi za kiuchumi.

“Tunaendelea kuhimiza wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini uwepo wa watu wasiowafahamu katika maeneo yao,” amesema.

“Tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria  niwaombe wananchi muendelee kutoa taarifa pindi mnapobaini wageni katika maeneo yenu, na wale mnaotaka watu wa kufanya kazi zipo taratibu za kufuata msiwaingize kiholela ni hatari kwa usalama wenu na wa nchi,” amesema Lyimo.

Baadhi ya wahamiaji waliokamatwa wamekiri kuingia nchini bila vibali wakitafuta maisha.

Mmoja wao, Bulimbu Seamadi, amesema ameishi Tanzania kwa miaka 20 bila kibali tangu alipokuja akiwa na umri wa miaka 13 na kwa sasa anafanya kazi kituo cha mabasi Geita kama mpiga debe na mkata tiketi.

“Nilikuja Tanzania kutafuta maisha nina wiki moja toka nitoke kwetu Burundi hali ya maisha huko ni ngumu ndio  maana tunaingia Tanzania kutafuta maisha , ni kweli tumekuja bila vibali shida ni kwamba hatuna hela ya kuomba vibali tunaomba mtupokee sisi sio watu wabaya,” amesema Senzalugeza Telas.

Takwimu za Idara ya Uhamiaji mkoani Geita zinaonyesha kuwa kati ya Julai hadi Agosti 11 mwaka huu  jumla ya wahamiaji haramu zaidi ya 300 kutoka Burundi, 14 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanne kutoka Uganda wamekamatwa mkoani humo.