Watatu Stars wakwepa mtego | Mwanaspoti

NYOTA watatu wa kikosi cha kwanza cha Taifa Stars, wamekwepa mtego wa adhabu ya kukosa mechi ijayo ya hatua ya makundi ya michuano ya CHAN 2024 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa jijijini Dar es Salaam.

Licha ya kuwa Stars ina uhakika wa kucheza robo fainali ya michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi ya ndani, ingekosa huduma ya kipa Yakoub Suleiman, kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji wake wa kati, Clement Mzize.

Nyota hao wangekumbana na rungu hilo kama wangeonyeshwa kadi za njano katika mechi iliyopita dhidi ya Madagscar ambayo Stars iliweka rekodi ya kushinda mechi ya tatu mfululizo kwa mabao 2-1  na kufikisha pointi tisa kwenye kilele cha kundi B.

Wachezaji hao kila mmoja alikuwa na kadi ya njano ambayo alionyeshwa kwenye mechi ya nyuma dhidi ya Mauritania ambayo Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika mechi iliyopita kiungo wa Stars, Yusuph Kagoma alinasa kwenye mtego huo na kukosekana kwenye mechi dhidi ya Madagascar jambo ambalo lilimfanya kocha wa kikosi hicho Hemed Suleiman ‘Morocco’ kumtumia Abdulrazack Hamza ambaye kiuhalisia ni beki wa kati. Hata hivyo alishindwa kumaliza mechi.

Kagoma atarajiwa kurejea katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Afrika ya Kati ambayo Stars itakuwa ikisaka kumaliza kinara wa kundi B baada ya kutinga mapema robo fainali.

Katika mechi ya Madagascar hakuna mchezaji hata mmoja wa Stars ambaye alionyeshwa kadi ya njano hivyo wanaenda kwenye mchezo ya mwisho kila mmoja akiwa safi.

Kanunia ya mashindano hayo inaelekeza mchezaji aliyeonyeshwa kadi ya njano katika mechi mbili mfululizo atakosa mechi inayofuata.