Tabora. Watoto 50 walionusurika katika ajali ya moto uliozuka katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Igambilo kilichopo katika kata ya Misha, Manispaa ya Tabora, wameendelea kupokea mahitaji muhimu kutoka kwa Serikali na wadau mkoani Tabora.
Watoto hao ni waathirika katika ajali hiyo ya moto iliyotokea Julai 29, 2025 na kusababisha vifo vya watoto watano wa kike waliokuwa wakilelewa katika kituo hicho.
Watoto hao wamehamishiwa katika kituo cha kulelea watoto cha Istiqaama kilichopo kata ya Malolo manispaa ya Tabora ili kuendelea kupata huduma muhimu na kurejesha hali yao ya kawaida huku wakisubiri maboresho katika kituo chao cha Igambilo kukamilika.
Akizungumza katika kituo hicho leo Agosti 12, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella amesema hali ya watoto hao kwa sasa ni nzuri na tayari amekabidhi baadhi mahitaji ikiwa ni michango ya Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa mkoani humo kama sehemu ya jitihada za kuendelea kurejesha mahitaji yao muhimu yaliyoteketea kwa moto.
“Tunashukuru kuwa tumekuta watoto hawa wanaendelea vizuri lakini wapo sehemu salama kabisa na sisi kama Serikali kwa kushirikiana na wadau tunaendelea kuhakikisha mahitaji muhimu yanapatikana na watoto hawa wasijisikie unyonge kutokana na matatizo yaliyowapata,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella akizungumza na watoto katika kituo cha Istiqaama kilichopo Kata ya Malolo Manispaa ya Tabora. Picha na Hawa Kimwaga
Amesema Serikali itaendelea kuwa karibu na watoto hao kuhakikisha wanakuwa na mazingira bora, lakini masomo yao yaendelee ili wasirudi nyuma kielimu kutokana na changamoto ambazo wamepitia kwa siku chache zilizopita.
Aidha, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora, Aisha Churu amebainisha kuwa miongoni mwa mahitaji ambayo wamekabidhi ni unga, mchele, sukari, mafuta ya kula, hijabu, maji, belo mbili za mitumba za nguo za watoto na taulo za kike.
Kwa upande wake, mlezi katika kituo cha kulelea watoto cha Istiqaama ambapo watoto hao wamehamishiwa kwa muda, Mwalimu Hadija Nassoro ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwafuatilia kwa ukaribu watoto hao na kwamba kwa sasa hali zao zinaridhisha tofauti na awali walikua na huzuni wakati wote.
Naye Hajira Ismail ambaye ni miongoni mwa watoto 50 kutoka kituo cha Igambilo waliohamishiwa kituo cha Istiqaama, ameishukuru Serikali na wadau ambao kuwakumbuka kuwa wana matatizo na kuwatafutia mahitaji.