Wazazi wakumbushwa kutowaruhusu watoto kushiriki michezo ya kubahatisha

Dar es Salaam. Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), imewaonya wazazi na walezi nchini kutowaruhusu watoto chini ya miaka 18, ushiriki wa michezo ya kubahatisha, ikiwemo Play Station.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi hiyo, Daniel OleSumayan leo Agosti 12, 2025, kwenye mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, ukiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu michezo ya kubahatisha nchini pamoja na kueleza majukumu ya bodi hiyo.

Amesema watoto hawaruhusiwi kushiriki michezo hiyo na wanapaswa kulindwa kushiriki hata kwa njia ya kiteknolojia, huku akisisitiza wajibu wa kwanza unaanzia kwa mzazi.

“Wazazi tunapaswa kuwalindwa watoto wetu, tujue wanafanya nini, katika vitu tunavyowanunulia katika kuwajengea uwezo wao na kuchangamsha bongo zao, ni vyema tuendelee kufuatilia wanafanya nini na vyombo hivyo.

“Kwa sababu michezo ya hizi Play station ambazo zinatumika kama michezo ya kubahatisha ni lazima iendeshwe katika maeneo maalumu ambayo bodi imeidhinisha. Kwa hiyo hilo tena tunaendelea kusisitiza kwamba tukae na watoto wetu ili tuweze kuwaongoza vizuri,” amesisitiza.

Hata hivyo, ikumbukwe mtu yeyote atakayeruhusu mtoto (chini miaka 18) kushiriki, kuingia, kuzunguka au kukaa katika michezo ya kubahatisha muhusika anahesabiwa kafanya kosa na atakabiliwa na kifungo cha miezi 12, faini ya Sh1 milioni na isiyozidi Sh5 milioni au vyote kwa pamoja.

Hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 70 cha sheria ya michezo ya kubahatisha. Michezo hiyo inaendeshwa kwa sheria ya michezo ya kubahatisha namba 4 ya mwaka 2003 sura ya 41 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Olesumayan amesema changamoto ni uwepo wa waendeshaji wasio na leseni ambao hawana usajili wa GBT hususan wa mashine za sloti maarufu dubwi, hivyo husababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

Ambapo mbali na hilo pia wanaendesha biashara hiyo kiholela katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria na hivyo kuleta usumbufu kwa jamii, ikiwemo kushiriki kwa watoto. Pia, bodi inaendelea kupambana na wageni wasiofuata sheria na wanaochezesha michezo hiyo kihalifu.

Pia, michezo ya kubahatisha hairuhusiwi kuendeshwa karibu na nyumba za ibada, shule, maeneo ya usalama na yale yasiyofikika kirahisi.

Akifafanua zaidi amesema wananchi kwa sasa wana mwamko kiasi cha kutoa taarifa wakiona mashine za michezo hiyo zimekaa sehemu isiyotakiwa kisheria, nao  wao kwa kushirikiana na vyombo kuzikamata na kuziharibu.

Takwimu zinaonesha nchini kuna   kampuni 62 za michezo ya kubahatisha zilizosajiliwa na bodi hiyo huku kukiwa na ongezeko la kodi kutoka Sh131 bilioni kwa mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh260 bilioni mwaka 2024/25 ikiwa ni ongezeko la asilimia 97.

Aidha, makusanyo ya kodi kwa jumla hadi mwaka 2024/25 ni Sh922 bilioni huku ufadhili, ajira na uwekezaji wa wageni ukiongezeka. Amesema ajira zinaongezeka kila mwaka hadi kufikia Juni, 2025 zimefikia zaidi ya 30,000 ikijumuisha rasmi na zisizo rasmi. Pia sekta imechangia Sh53 bilioni kuendeleza michezo nchini. Uwekezaji kutoka nje ukifikia Sh66.7 bilioni

Katika hatua nyingine bodi hiyo inawalinda watu wanaoonekana kuwa waraibu wa michezo ya kubahatisha wale wanaotumia pesa bila mpangilio, kugombana na familia, kuuza rasilimali na kutoshiriki kazi.

Amesema katika miaka minne nyuma sekta hiyo imekuwa ikikua kwa asilimia 18.6 ikiwa juu ya wastani wa kawaida. Huku akisema michezo hiyo ni burudani na ushindi hupatikana kwa bahati tu ila kwa wachezaji, waendeshaji ni biashara na kazi.

Amesema ni kinyume cha sheria kuendesha biashara ya michezo ya kubahatisha bila kuwa na leseni hai inayotolewa na GBT ambazo hutolewa kila mwaka kisha kuhuishwa kwa mtu mwenye sifa.