22 wakwama mgodini, watatu waokolewa

Shinyanga. Watu 22 ambao ni wafanyakazi na mafundi mgodini wamefukiwa kwenye mashimo baada ya kutitia wakati wakifanya ukarabati na watatu miongoni mwao wameokolewa.

Chifu Inspekta wa kikundi cha wachapakazi Gold Mine, Fikiri Mnwagi ambao ni wamiliki wa mgodi huo, amesema kuwa maduara hayo matatu yalikuwa katika ukarabati hali iliyopelekea ardhi ya eneo hilo kutitia na kuwafunika.

Ajali hiyo ilitokea katika mgodi wa kikundi cha wachapakazi uliopo katika Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Agosti 11, 2025 saa nne asubuhi, mawasiliano yaliyokuwa yakifanyika kati ya watu 6 wa duara namba 106 yameleta matunda na watu watatu wameokolewa jana Agosti 12, 2025 shughuli ya uokoaji bado inaendelea.

“Duara namba 106 walikuwa watu 6 ambao tulifanyikiwa kufanya mawasiliano nao kwa sauti ya mwangwi na kuokoa watu watatu, huku duara namba 20 na 103 hatujafanyikiwa kufanya nao mawasiliano lakini juhudi Bado zinaendelea na tumechimba duara la ziada ili kuweza kuwafikia wengine pamoja na kupitisha maji na chakula,” amesema Mnwagi.

Akizungumza Agosti 12, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro baada ya kufika eneo la tukio amewaomba wananchi wawe watulivu zoezi la uokoaji bado linaendelea huku lengo kuu likiwa ni kuwaokoa watu wote na kufanya juhudi za kupata mawasiliano na wengine pia,

“Watu 25 walifukiwa na watatu tayari wameokolewa huku maduara mawili bado hatujafanyikiwa kupata mawasiliano nao lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha pia tunapata mawasiliano na kuwaokoa wote, duara namba 20 lina watu nane, 103 watu 11 na 106 watu sita na mpaka sasa tumeokoa watatu,” amesema Mtatiro.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amefika eneo la tukio na kuzungumza na wananchi na wafanyakazi wa eneo hilo na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki  wa eneo hilo na kutoa shukrani kwa wakazi wa eneo hilo kwa juhudi za awali za uokoaji.

“Watu wa mgodi huu wanaujirani mwema kwa sababu tangu tukio hili limetokea mafundi wa migodi jirani wameweka kambi eneo hili kuhakikisha zoezi zima la uokoaji linaenda vizuri nawashukuru sana kwa sababu waokoaji wa kwanza ni wakazi wa eneo husika,” amesema Mhita.

Nao baadhi ya wakazi na wafanyakazi wa eneo hilo akiwemo Joseph Shahibu ameeleza kuwa wapo vijana wengi wenye nguvu na wanaweza kuchangia katika uokoaji wanaomba kuruhusiwa katika kushiriki katika uokoaji na pia anaomba kasi ya uokoaji iongezwe.

“Tunashukuru kwa juhudi za uokoaji ambazo zimefanywa na zinaendelea kufanywa lakini ombi langu ni kuruhusu baadhi yetu kupewa nafasi ya kushiriki katika zoezi la uokoaji kwa sababu tuna nguvu na tunaweza kuchangia katika uokoaji” amesema Shahibu.