TIMU ya Taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati imeendelea kugawa pointi za bure katika michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), baada ya kukubali tena kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Madagascar.
Katika mechi hiyo ya kundi B iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilicheza vizuri kuanzia mwanzo japokuwa mwishoni ilizidiwa ujanja na wapinzani wake na kukubali mabao ya dakika za jioni.
Madagascar ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 84 lililofungwa na ‘super sub’ Toky Rakotondraibe aliyeingia dakika ya 78 kichukua nafasi ya Jean Ranaivoson, huku la pili likifungwa na Lalaina Cliver Rafanomezantsoa dakika ya 90.
Kwa matokeo hayo yanaifanya Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchapwa mechi zote tatu ilizocheza baada ya kichapo cha mabao 4-2 dhidi ya Burkina Faso ikachapwa tena bao 1-0 na Mauritania na leo kupoteza pia 2-0, mbele ya Madagascar.
Kwa upande wa Madagascar huu ni ushindi wake wa kwanza katika michuano hii baada ya kuanza kwa suluhu dhidi ya Mauritania, huku mechi ya pili ikikutana na kichapo cha mbao 2-1 mbele ya waandaji wa mashindano hayo, Taifa Stars.
Katika kundi B timu ya Taifa ya Taifa Stars ambayo imekata tiketi ya kucheza robo fainali inaongoza ikiwa nq pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu ikifuatiwa na Madagascar na Mauritania zenye pointi nne zikiwa nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.
Burkina Faso inayoshuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa muda mfupi ujao kuanzia sasa kupambana na Mauritania, inashika nafasi ya nne na pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili, huku Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiburuza mkiani bila pointi.