Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ilani yake ya uchaguzi, kimeweka dira ya inayolenga kubadilisha mfumo wa afya wa Tanzania.
Katika ilani hiyo, neno “afya” limetajwa mara 63 kama kiini cha mikakati ya kisera, kitaalamu na kimfumo.
Mpango huu unagusa nyanja zote muhimu—kuanzia miundombinu, rasilimali watu, dawa na vifaa tiba, hadi mifumo ya kugharamia na teknolojia itakayotumika, ili kufikia lengo la huduma bora kwa Watanzania wote, Bara na Zanzibar.
Hatua zilizopigwa miaka minne
Katika kipindi cha 2020 hadi 2024, takwimu zinaonyesha mabadiliko makubwa katika afya ya mama na mtoto.
Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 104, upungufu wa zaidi ya asilimia 80.
Vifo vya watoto wachanga navyo vimeshuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000. Mabadiliko haya yanahusishwa na maboresho katika huduma za kabla, wakati na baada ya kujifungua, pamoja na kupanua wigo wa chanjo na huduma za kinga.
Hata hivyo, CCM inakiri kuwa safari haijaisha. Viwango bora vya kimataifa bado havijafikiwa, na mikakati mipya imewekwa ili kuongeza kasi ya maboresho haya.
Huduma zinasogezwa karibu na wananchi.
Katika kipindi cha miaka minne, vituo vipya 1,288 vya afya vimejengwa – zahanati 947, vituo vya afya 277, hospitali za halmashauri 57, hospitali za mikoa minne na hospitali tatu za kanda.
Lengo ni kupunguza umbali wa kufuata huduma, hasa vijijini ambako wananchi wengi waliwahi kutembea kilomita kadhaa kufika hospitali.
Zanzibar nayo imenufaika kwa ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, ujenzi wa hospitali mpya za mikoa, kuboresha maabara za afya ya jamii na kuanzisha hospitali ya magonjwa ya akili kisiwani Pemba.
Uhakika wa dawa na vifaa tiba
Kiwango cha upatikanaji wa dawa muhimu kimepanda kutoka asilimia 75.6 mwaka 2020 hadi asilimia 89.3 mwaka 2024.
Hii inamaanisha karibu dawa tisa kati ya 10 zinazohitajika zinapatikana kwa wakati. Serikali imeimarisha Bohari ya Dawa (MSD) na kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kuanzisha viwanda vya bidhaa za afya, kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.
Mapambano dhidi ya malaria
Malaria bado ni tishio kubwa. Asilimia nane ya Watanzania huambukizwa na ugonjwa huo kila mwaka (asilimia 10 vijijini na asilimia moja mijini) na nchi inachangia asilimia 4.4 ya vifo vyote vya malaria duniani.
Mpango wa CCM ni pamoja na kuangamiza mazalia ya mbu nchini kote, kuimarisha kiwanda cha kuzalisha dawa cha Kibaha, na kuhakikisha kila halmashauri inatenga bajeti mahsusi kwa kazi hiyo.
Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inalenga kutoa kinga ya kifedha dhidi ya gharama za matibabu kwa kila Mtanzania.
Zanzibar, kupitia Mfuko wa Huduma ya Afya, inalenga kuongeza usajili wa wanufaika na kufikia “Universal Health Coverage.”
Hatua hii inaweza kupunguza hatari ya wananchi kuingia kwenye umasikini kutokana na gharama za ghafla za matibabu.
Rasilimali watu katika mfumo wa afya
Uhaba wa wataalamu wa afya, hasa wabobezi, umetambuliwa kama changamoto.
CCM inalenga kuongeza idadi yao na kuboresha uwiano wa daktari kwa wagonjwa kutoka daktari mmoja akihudumia wagonjwa 6,272 hadi daktari mmoja atahudumia wagonjwa 3,100.
Pia kunatarajiwa kuimarishwa huduma za afya ya akili, msaada wa kisaikolojia na kuimarisha tiba asili ikiwamo kilimo cha mimea dawa.
Mifumo ya kidijitali na akili unde
Kuanzishwa kwa mifumo ya kidijitali na matumizi ya akili mnemba (AI) katika uchunguzi na matibabu utaboresha usahihi wa vipimo na kuongeza kasi ya huduma.
Wahudumu wa afya watatumika kufikia wananchi walioko maeneo ya mbali, kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma kwa sababu za kijiografia na usafiri.
CCM imeweka mikakati ya lishe kwa wanafunzi wa shule za maandalizi na msingi, pamoja na kuimarisha utoaji wa chanjo na huduma za kinga.
Zanzibar inalenga kupunguza vifo vya watoto kabla ya kuzaliwa na katika mwezi wa kwanza wa maisha hadi 26 kwa kila vizazi hai 1,000.
Michezo na utamaduni pia vimehusishwa kama njia za kuboresha afya ya jamii, kwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kimwili.
Changamoto na utekelezaji
Changamoto za utekelezaji wa Ilani ya CCM katika sekta ya afya zinahusisha vikwazo vya kifedha, miundombinu na rasilimali watu.
Licha ya mipango ya kujenga na kukarabati vituo vya afya kote nchini, changamoto ya uhaba wa bajeti thabiti na ya kutabirika inaweza kuathiri mipango hii.
Miradi mingi ya afya inategemea mgawo wa fedha kutoka serikalini, ambao unaweza kuathiriwa na changamoto za kiuchumi au mabadiliko ya vipaumbele vya kitaifa.
Gharama za kuendesha vituo hivi, ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya wataalamu wa afya na kununua dawa na vifaa tiba, zinaweza kuathiri kasi na ubora wa huduma endapo hazitapangiwa rasilimali ipasavyo.
Pia, upungufu wa wataalamu wa afya wenye ujuzi wa kitaalamu unaweza kuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa ilani.
Lengo la kupunguza uwiano wa daktari kwa wagonjwa linaweza kukwama iwapo juhudi za kuongeza ajira, mafunzo na mazingira bora ya kazi hazitafanikishwa.
Kokosa wahudumu wa afya pamoja na changamoto za kutunza wataalamu waliopo, unaweza kufanya vituo vipya vya afya kutofanya kazi ipasavyo.
Pia, sekta ya afya ya akili na tiba asili, ambazo zimepewa kipaumbele, zinaweza kukwama kutokana na kukosa utaalamu maalumu na miundombinu ya kitaalamu.
Akizungumzia hilo, mtaalamu wa afya, Aminieli Swai anasema licha ya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali na matumizi ya akili mnemba (AI), kuna hatari ya teknolojia hizo kutoleta matokeo yanayotarajiwa endapo hakutakuwa na mafunzo ya kutosha, usimamizi wa kitaalamu na miundombinu ya Tehama iliyo imara.
Anasema mapambano dhidi ya magonjwa sugu kama malaria na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi, mashirika ya kijamii na wananchi.
“Bila ushirikiano huo na bila kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za afya kutoka nje, malengo ya ilani yanaweza kubaki kwenye maandiko bila kutekelezwa kikamilifu,” amesema Swai.
Ilani inaonyesha picha ya matumaini, lakini changamoto kubwa, kama zilivyoelezwa hapo juu, zitakuwa kwenye utekelezaji endelevu wa miradi.
Naye Angela Bwaya, mfamasia kitaalumua, anasema bajeti thabiti, usimamizi wa karibu na ushirikiano wa sekta binafsi na wananchi ni nguzo muhimu.
Anasema ili CCM iweze kufanya mabadiliko chanya katika sekta ya afya kulingana na ilani yao, wanapaswa kuyasimamia malengo yaliyowekwa kwa umakini mkubwa, bila kufanya hivyo, yanaweza kubaki kwenye karatasi mpaka miaka mitano inamalizika.