AMRI JUU YA KESI YA LISSU KURUSHWA MUBASHARA KUTOLEWA AGOSTI 18

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imesema Agosti 18,2025 itatoa amri kuhusu kurushwa mubashara kwa maelezo ya mashahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Tundu Lissu.

Pia Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo kwa sasa amesema, siku hiyo upande wa Jamhuri utamsomea mshtakiwa Lissu maelezo ya kesi ((Commital) ili kesi iweze kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Hatua hiyo inakuja kufuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu wa kubariki mashahidi ambao ni raia katika kesi hiyo kufichwa ili kulinda usalama wao.

Mapema katika kesi hiyo leo Agosti 13,2025 Wakili wa serikali Mkuu Nassoro Katuga aliikumbusha mahakama juu ya uamuzi wa mahakama kuu uliotolewa Agosti 4, ambao ulitoa amri mbali mbali sita ikiwemo vyombo vya habari kutoruhusiwa kutangaza mubashara taarifa za mashahidi ambao ni raia (commital) na ushahidi wakati wa usikilizŵaji wa kesi

Akiwasilisha hoja hiyo mbele ya Hakimu Kiswaga wakili Katuga alidai kuwa ingawa Mahakama Kuu imeruhusu matumizi ya mashahidi wa siri, bado kuna haja ya kuweka zuio la kurusha mwenendo wa kesi mubashara wakati wa ushahidi wa mashahidi hao.

Katuga alidai kuwa kurusha mwenendo huo moja kwa moja ni sawa na kufanya uchapishaji (publication) wa ushahidi, jambo ambalo litakuwa kinyume na amri ya Mahakama inayolenga kulinda usalama na utambulisho wa mashahidi hao.

Aliongeza kuwa kwa kuwa ushahidi huo utatolewa kwa namna ya siri, kuwepo kwa matangazo ya moja kwa moja kunaweza kusababisha mashahidi kutambulika kupitia maelezo yao, hivyo kuhatarisha ulinzi wao.

Akijibu hoja hizo, Lissu alidai kuwa anafikiri Wakili Katuga anatanua amri iliyotolewa na Jaji Hussein Mtembwa kufunika mambo mengine ambayo hayajakatazwa.

Kuhusu hoja ya kwamba kesi isiwe mubashara , Lissu alidai kuwa ni hoja ambayo haijaamuliwa na Jaji yeye kasema amekataza kile ambacho kitamfichua shahidi.

“Katika hoja ya kwanza, Jaji Mtembwa alisema utambulisho wao hautatolewa hadharani majina, anuani zao wala mahali wanapokaa na hata tutakapokwenda Mahakama Kuu,”alidai Lissu

Alidai Jamhuri wanachotakiwa kukifanya kulingana na amri hizo ni kuchuja ushahidi wa mashahidi wao kwa kuficha taarifa zao binafsi ili mashahidi wao wasijulikane, lakini siyo kusema kesi isirushwe mubashara.

“Kuomba hoja ambayo haijaamuliwa na Jaji hiyo haiwezekani kwa sababu yeye alisema kisitangazwe kile kitakachoonesha utambulisho wa mashahidi na pia tayari mmeshaondoa taarifa zao kwenye nyaraka, shida iko wapi hapo,”? Alihoji Lissu

Katika kesi hiyo inadaiwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam mshtakiwa Lissu akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam alitangeneza nia ya kushawishi au kuchochea umma ya kuweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kusema maneno yafuatayo

“Walisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi tutahamasisha uasi, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko….kwa hiyo tunaenda kukinukisha sanasana huu uchaguzi tutaenda kuvuruga kwelikweli, tunaenda kukinukisha vibaya sana,”.