Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
MGOMBEA Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Siasa cha Democratic Party (DP),Abdul Mluya,amesema endapo chama hicho kitapata nafasi ya kuongoza Nchi moja ya kipaumbele chao ni kwenda kusimamia suala la Kikokotoo.
Mluya ambaye aliambatana na mgombea mwenza Saodun Abraham Khatibu ameyazungumza hayo mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliopo jijini Dodoma.
Amesema suala la Kikokotoo kwa watumishi imekuwa changamoto kubwa sana kwa watumishi hivyo DP inakwenda kulifanyia kazi suala hilo ili watumishi waweze kupata mafao yao bila changamoto yeyote
“Tunakwenda kufuta kilio cha Kikokotoo kwa watumishi,haiwezekani mtu afanye kazi ndani ya miaka 33 halafu alipwe mafao sh milioni 13 hadi 14 hilo tunakwenda kuliondoa,”amesema Mluya.
Amesema serikali ya DP itakwenda kuwajengea nyumba watumishi ambao wamekaa ofisini zaidi ya mwaka bila kashfa ya kosa lolote lile ili kusaidia kuondoa rushwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mbali na hayo pia amesema DP itashughulikia na kuboresha maslahi ya Jeshi la Magereza pamoja na majeshi mengine ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora na kuongeza kuwa wataboresha pia suala zima la Magereza ya wafungwa hapa nchini.
Mluya amesema vipaumbele vingine kwao ni suala la Afya,ambapo kinamama watajifungua bure na mtoto atapewa lishe kwa miezi mitatu huku akisema marehemu hatadaiwa hela ya matibabu,ndugu watapewa mwili ili wakazike na kwenye kilimo watahimiza kilimo cha umwagiliaji.