Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Benki ya Dunia kuhusu Nishati Safi ya Kupikia (World Bank Multi-Tier Framework – MTF, 2020) Nishati safi ya kupikia hupimwa kwa kuzingatia ufanisi, urahisi wa kutumia, upatikanaji, usalama, unafuu wa gharama na kiwango kidogo cha sumu kinachotolewa wakati wa matumizi.
Lengo kuu ni kuhakikisha nishati hiyo inakuwa salama kiafya, inapatikana kwa urahisi na haina madhara makubwa kwa mazingira.
Vilevile, Mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa mwaka 2021 umefafanua viwango vya nishati safi ya kupikia kwa kuangalia chembechembe ndogo (PM2.5) na kiwango cha gesi ya kaboni monoksidi (CO) inayozalishwa.
WHO inabainisha kuwa kiwango cha PM2.5 kisizidi microgramu 5 kwa mita ya ujazo kwa mwaka, au kiwango cha mpito cha microgramu 35 kwa mwaka, na CO isiwe zaidi ya miligramu 4 kwa mita ya ujazo ndani ya saa 24.
Kwa uhalisia kiwango cha PM2.5 na CO kinachotokana na mkaa kinategemea aina ya mkaa, ubora wa kuchoma na uingizaji hewa.
Kwa kawaida, matumizi ya mkaa majumbani huzalisha PM2.5 zaidi ya microgramu 100 hadi 500 ambazo ni zaidi ya mara 14 hadi 20 ya kiwango hitajika, na kiwango cha CO kinachozalishwa ni miligram 10 hadi 30 ambazo ni mara mbili hadi tisa ya kiwango pendekezwa.
Kwa Tanzania, Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaeleza kuwa nishati safi ni ile inayotumika kwa usahihi na kutoa moshi wenye kiwango kidogo cha sumu, huku ikihakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji, kuokoa muda, kupunguza gharama, athari za kiafya na kimazingira.
Aina za nishati safi ya kupikia
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia (2023) na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024). Nishati na teknolojia safi zinazoidhinishwa kitaifa na kimataifa ni pamoja na umeme, gesi, bayogesi nishati zitokanazo na vyanzo jadidifu.
Tukisema nishati jadidifu tunamaanisha nishati inayotokana na vyanzo vinavyoweza kujizalisha upya kiasili na kwa kasi, bila kuisha, mfano, jua, upepo, maji, mawimbi, jotoardhi (geothermal), na biomasi endelevu.
Na vyanzo visivyo salama ni vile vinavyotokana na nishati tongamotaka ambapo vyanzo vyake vinavyopungua na kuisha kadri vinavyotumika, kwa kuwa havijizalishi tena kwa muda mfupi, mfano ni makaa ya mawe, mafuta ya petroli, gesi asilia na urani kwa nyuklia. Vyanzo hivi vina tabia ya uchafuzi wa mazingira japo kiwango cha uchafuzi kunatofautiana.
Nishati safi ya kupikia inaweza kutoka kwenye umeme. Chanzo hiki hakina moshi na ni salama kiafya. Pia kuna majiko umeme, jiko la miale ya sumakuumeme (induction cookers) na hotplates. Umeme hupunguza hatari za moto na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba.
Bayogesi ni chanzo kinachozalishwa kutokana na uchakataji wa kinyesi cha wanyama, mabaki ya vyakula au mimea bila hewa ya oksijeni. Inatumika kwa majiko ya gesi ya nyumbani na taasisi kama shule na hospitali.
Hii pia ina fursa kubwa kwenye mazingira kwani zinazalishwa taka nyingi kila siku. Mfano inakadiriwa zaidi ya tani 5,200 za taka huzalishwa kila siku mkoani Dar es Salaam, lakini asilimia kubwa ya taka hizi huishia dampo la Pugu.
Chanzo kingine ni bayoethano, nishati ya kioevu inayopatikana kutokana na uchachushaji wa mazao yenye wanga kama miwa na nafaka. Hutumika kwa majiko maalumu yanayofanana na ya petroli lakini salama zaidi kiafya. Chanzo hiki ni maarufu zaidi kwenye viwanda vya miwa nchini.
Nishati ya jua pa hutumika kwa majiko ya sola yanayobadilisha mionzi ya jua kuwa joto la kupikia, hususan katika maeneo yenye mwanga wa kutosha.
Majiko banifu ni yale yanayotumia kuni au mkaa kwa ufanisi zaidi na kutoa moshi kidogo, mfano majiko ya chuma yenye sehemu ya kudhibiti moshi na joto. Haya hupunguza matumizi ya mkaa na kuni sio kuacha kabisa matumizi.
Mkaa mbadala pia ni suluhu nyingine kwani hutengenezwa kutokana na masalia kama pumba za mpunga, majani makavu, maranda ya mbao au takataka ngumu na kuchanganywa na vifungio ili kutoa nishati yenye moshi mdogo.
Nyingine ni gesi ya LPG (Liquefied Petroleum Gas), hii ni ile inayohifadhiwa kwenye mitungi na kutoa muwako safi bila moshi mwingi. Mfano matumizi ya mitungi ya kilo sita au 15 yenye majiko ya sahani moja au mbili, inayopatikana mijini na baadhi ya vijiji.
Gesi asilia ni chanzo kinachotolewa kupitia mabomba kutoka vyanzo kama Songosongo na Mnazi Bay. Inatumiwa moja kwa moja majumbani kupitia majiko maalumu na ina kiwango kidogo cha gesi chafu. Zipo zaidi ya nyumba 1,500 zilizoungwa na gesi hii katika mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam na Lindi.
Hata hivyo kitaalamu gesi si nishati safi, lakini ina afadhali katika kuleta uchafuzi kwa mazingira na madhara ya afya ikilinganishwa na kuni na mkaa zenye athari zaidi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, teknolojia hizi huchaguliwa kulingana na upatikanaji wa malighafi, gharama, urahisi wa usambazaji na uwezo wa watumiaji kumudu gharama za awali na uendeshaji.
Hata hivyo changamoto kubwa inabaki kuwa unafuu, urahisi wa upatikanaji, matumizi pamoja na uelewa. Nyingi ya nishati hizi zina gharama kubwa na hivyo moja kwa moja zinakinzana na tafsiri ya nishati safi ya kupikia kama tulivyoona mwanzoni.
Licha ya ukweli kwamba yapo madhara ya kiafya na mazingira lakini sababu kubwa ya matumizi ya mkaa na kuni ni unafuu na urahisi wa upatikanaji wake ambao vyanzo vingine safi havina.
Japo zipo tafiti zinazoonyesha matumizi ya mkaa na kuni yana gharama zaidi kuliko vyanzo vya nishati safi. Inawezekana lakini ni suala la mjadala mpana kidogo.
Hali ya matumizi nchini Tanzania, umuhimu wake
Takwimu za Benki ya Dunia (WB) zilizotolewa 2023 zilionyesha kuwa mwaka 2021 ni asilimia 6.9 pekee ya Watanzania waliokuwa wakitumia nishati safi ya kupikia, ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 71. Takribani asilimia 90 ya kaya bado hutegemea kuni na mkaa kama nishati kuu, huku matumizi ya kuni yakifikia asilimia 63.5 na mkaa asilimia 26.2 kwa mujinu wa Cooking Energy Action Plan ya mwaka 2022.
Licha ya uhalisia huo bado nishati safi ya kupikia ni suluhisho na imethibitishwa kuwa na uwezo wa kulinda afya kwa kupunguza moshi wenye sumu, inalinda misitu kwa kupunguza ukataji miti, inaokoa muda wa kutafuta kuni, na inapunguza gharama za matibabu. Pia, ni nyenzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.
Jitihada za kitaifa na kimataifa
Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Hatua hii inatekelezwa sambamba na malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa ya kidunia hususan lengo namba saba (SDG 7) linalokusudia kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, salama na endelevu kwa wote. Lakini pia ni sambamba na masharti ya Mkataba wa Paris (2015) ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.
Kwa kujifunza kutoka mataifa mengine, Tanzania imeanzisha miradi ya ruzuku na mikopo nafuu kwa kaya zenye kipato cha chini, kushirikisha sekta binafsi katika usambazaji wa gesi, na kuchunguza fursa za biashara ya kaboni kufadhili miradi ya nishati safi.
Mwananchi itaendelea kuchambua zaidi undani wa haya na uhalisia kwenye maisha ya Watanzania. Endelea kufuatilia maudhui haya.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.