Hakuna asiyeijua homa. Kupanda kwa homa kunaambatana na athari kadhaa mwilini: Joto la mwili litaongezeka, atatapika au hata na kuharisha.
Kichwa kitamgonga na atapatwa na athari nyingine chungu nzima kulingana na mgonjwa mwenyewe. Mwili utakuwa na maumivu kiasi cha kushindwa kufanya kazi kama ipasavyo. Joto la mwili linapanda kama kiazi kilichochemshwa jikoni. Kuna nyakati nilizowahi kupatwa na homa, nikakimbilia katika kituo cha afya. Mara zote nilikuwa nikimlalamikia daktari kwamba nilikuwa na malaria.
Lakini mara zote daktari aliniambia kwamba maelezo yangu ndiyo yatakayompa mwongozo wa kipimo ninachotakiwa kufanya.
Hicho ndicho kitakachothibitisha iwapo ni malaria kwani homa si ugonjwa, ila ni dalili ya ugonjwa. Inawezekana ikawa ni Malaria, lakini pia inawezekana ni ugonjwa tofauti
Watoto huwa wana shida zaidi kwani hawawezi kujieleza pale wanapoumwa. Kwa bahati nzuri wazazi wake wanapata shaka juu ya mabadiliko yake.
Watamwona asiye na makeke kama ilivyo kawaida yake, na akiwa na joto kali mwilini. Mama atamgusa shingoni kwa kutumia mgongo wa kiganja chake.
Hisia zake zitaamua iwapo kumpa mtoto huduma ya kwanza au kumkimbiza Hospitali akapate kipimo. Nchi yetu ina homa ya Uchaguzi Mkuu inayozidi kupanda.
Kadiri tunavyoisogelea siku hii adhimu ya kupiga kura, kumekuwa na ongezeko la joto miongoni mwa jamii ya Watanzania.
Hofu hii inatokana na matukio haramu yanayozidi kuongezeka kadiri siku inavyokaribia. Taifa linaonesha wazi kupadwa na joto kali na linahitaji huduma ya kwanza kama siyo kutibiwa.
Homa ya uchaguzi inatia hofu kwani hatujui ni ugonjwa gani unaoikabili nchi yetu. Inaweza kuumba mambo ya kufikirika yasiyo mazuri. Ni kawaida ya mtu mwenye hofu ya kurogwa, kuwa na hakika ya jambo hilo hata kama atapatwa na matatizo ya kawaida.
Mtu aliyepatwa na ajali baada ya kutishiwa maisha yake, huweza kudhani ajali hiyo ina mahusiano na vitisho alivyopitia. Hivi karibuni kumekuwa na habari nyingi za watu kupotea kwenye mazingira ya kutatanisha, habari hizi hivi sasa zimehamia kwenye homa ya Uchaguzi Mkuu. Watu wamefikia hatua ya kuandamana wakidai warudishiwe watia nia wao waliopotea. Tangu kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kulikuwa na sintofahamu miongoni mwa wapiga kura.
Hii ilitokea baada ya madai ya wananchi kulazimishwa kuchagua wagombea wasio machaguo yao. Inamaanisha kuwa watu wamepoteza imani miongoni mwao, wengine wanadhani kuwa kuna vikundi vinachowafanyia hujuma.
Mbaya zaidi hawajui vikundi hivi vinapokea maagizo kutoka wapi. Hivi sasa tukielekea Uchaguzi Mkuu, utata umeshika kasi kama au kuliko mwanzoni. Bila shaka haya yanatokea kwa sababu malalamiko ya awali hazikufanyiwa kazi ipasavyo.
Baadhi ya wapigakura walipinga mchujo wa majina ya watiania kwenye nafasi za udiwani na ubunge. Baadhi ya maeneo mamlaka zililazimika kurudia michakato, lakini sehemu zingine wamefunika kombe.
Hili si jambo la kubeza hata siku moja. Ndio maana nilisema katika barabara ya uchaguzi, kila penye shimo ni lazima pafukiwe.
Vurugu nyingi tunazozisikia kwa majirani zetu zinatokana na matatizo ya uchaguzi. Iwapo hatua za uhakika na uangalifu zitachelewa au kutowafikia walengwa, si ajabu kabisa mzimu ukahamia kwetu. Hao tunaowasikia wakipigana walikuwa watulivu kama sisi pale mwanzoni.
Wakati tupo kwenye huzuni ya kuondokewa na Spika mstaafu wa Bunge, tunaona video zinazodaiwa kuchukuliwa katika Jimbo la Kongwa alilokuwa akilitumikia.
Video hizo zinaonesha baadhi ya wanajimbo wakicheza ngoma kwa furaha wakati wakiushangilia msiba huo.
Hili nalo linahusishwa na figisu za kisiasa kwa namna marehemu alivyostaafu na alivyopita kwenye kura za maoni. Ni wajibu wa mamlaka kufanya uchunguzi. Kama ni kweli, hatua kali za haraka zichukuliwe kama alivyoahidi Mkuu wa Wilaya ya Kongwa. Watanzania hatuna utamaduni kama ule hasa kwenye mambo yanayogusa jamii.
Lakini hata kama ni uzushi hatua zichukuliwe kwa wazushaji. Taarifa ya uchunguzi iwekwe bayana ili kuepusha taharuki, na kuzuia kujirudia tena kwa hali kama hiyo katika mahala pengine.
Bila shaka wapo wanaonufaika na hofu kama hii. Kwenye madhara kama mafuriko au tetemeko la ardhi wapo wanaofaidika. Kwa vyovyote wezi watakuwa wafaidika wa kwanza. Pia kuna wale watakaotumia nguvu zao kuwaokoa wengine.
Lakini msisahau Kama nao wataachiwa waendelee na ubabe wao, lolote litakalowatokea wateule hawa (hata kama ni la kawaida) litaongeza tabaka la hofu kwenye jamii nzima.
Chama tawala kinapaswa kuwa na umakini wa hali ya juu kwenye michakato yao Hiki kinapaswa kuwa mfano wa kuigwa na vyama vingine vyote. Kazi ya kambi ya upinzani ni kurekebisha mapungufu ya Serikali iliyoundwa na chama hiki.
Kelele na malalamiko ya wanachama wao yanatoa mwangwi kwa Watanzania wote. Sintofahamu zinazoendelea kujitokeza zitasababisha hali isiwe tulivu, kwa kuwa wapinzani watazikosoa wakati wenyewe wanazilea.
Itakuwa ni namna ya kuongeza joto tusilojua linatuashiria gonjwa gani siku zijazo.