Jeuri ya pesa, Fei akiamua hatima yake

JEURI ya pesa! Hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ameshafanya uamuzi wa wapi atakipiga msimu ujao na kinachoelezwa ni kwamba fedha imeongea zaidi.

Mchezaji huyo amekuwa akitakiwa na timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi ikiwamo Simba na Yanga kwa hapa nchini na pia timu yake, Azam FC huku nje ikitajwa zaidi Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayonolewa na aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Nasrredine Nabi.

Hata hivyo, Fei ameamua kuchagua kuendelea kuitumikia Azam FC kwa mwaka mmoja zaidi akidaiwa kulamba dau la Sh800 milioni.

Kiungo huyo ambaye alijiunga na Azam FC akitokea Yanga alibakiza msimu mmoja tu kuwa mchezaji huru baada ya kutumikia timu hiyo kwa misimu miwili, hivyo kusaini kwake kandarasi ya mwaka mmoja anajifunga kwa misimu miwili zaidi.

Ipo hivi; Fei Toto alikuwa anatajwa kujiunga na Simba au Yanga katika dirisha hili, lakini mambo yamekuwa magumu zaidi baada ya uongozi wa Azam FC kumshawishi kubaki ndani ya timu hiyo kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani inayodaiwa kuwa ni Sh800 milioni kwa mwaka mmoja.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Azam FC kimeiambia Mwanaspoti kuwa Fei Toto bado ataendelea kuitumikia timu hiyo hadi 2027 na hii ni baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja ambao umekuwa na vipengele vitatu – ikiwamo kupewa dau nono la usajili na kuongezewa mshahara ambao unadaiwa kuwa atakuwa analipwa zaidi ya Sh70 milioni kwa mwezi.

Kimesema mshahara wa mchezaji huyo umepanda kutoka Sh50 milioni aliokuwa analipwa awali na pesa ya usajili imefikiwa milioni 800 baada ya makubaliano ya pande zote mbili.

“Tajiri amevunja benki amembakiza Fei Toto kwa mwaka mmoja, hivyo bado ana miaka miwili kuanzia msimu huu na msimu ujao nafikiri. Huu ni usajili mkubwa uliofanyika tena kwa gharama kubwa kutokana na mchango mkubwa wa mchezaji huyo, ukiondoa ongezeko la mshahara pia ubalozi wa Azam Pesa ambao awali alikuwa analipwa 150 milioni sasa atapata 200 milioni kwa mwaka,” kilisema chanzo na kuongeza:

“Kumpoteza mchezaji muhimu kama Fei Toto lisingekuwa suala zuri, lakini mara baada ya kocha kuweka wazi kuwa bado anahitaji huduma ya mchezaji huyo ndani ya kikosi cha Azam FC kutokana na uwezo mkubwa alionao uongozi umefanya jidihada za ushawishi mkubwa wa fedha na kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja.”

Chanzo hicho kilisema uongozi umetambua umuhimu wa kiungo huyo na kuamua kukaa naye chini na kukubaliana kusaini mkataba mpya wanaamini uwepo wake ni chachu ya mafanikio kibiashara na kiutendajni.

Haijafahamika zaidi ni kiasi gani amepewa mchezaji huyo, lakini imethibitika kuwa amepewa dau nono la usajili wa mwaka mmoja sambamba na kuongezewa fedha ya mshahara kwa mwezi.

Nyota huyo ambaye alijiunga na Azam FC akitokea Yanga tayari ameitumikia kwa misimu miwili ambapo msimu wa kwanza aliisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya pili akiichangia mabao 19 na asisi tatu, msimu wa pili ambao ni uliopita amefunga mabao manne na asisti 13.

Ukiondoa ofa ya Simba na Yanga aliyokuwa nayo kiungo huyo pia alishawishiwa na aliyewahi kuwa kocha wake mkuu ndani ya kikosi cha Yanga, Nasreddine Nabi ili atue Kaiza Chief mambo hayajaenda sawa pia.