KITENDO cha kocha mpya wa Azam FC, Florent Ibenge katika kikosi chake kuwepo na viungo wakabaji saba, kimetafsiriwa katika sura mbili tofauti kikosi kipana na kubalansi timu.
Viungo wakabaji waliopo Azam hadi sasa ni Sospeter Bajana, Sadio Kanouté, Himid Mao,Yahya Zayd, Ever Meza, Adolf Mtasingwa na James Akaminko, jambo ambalo Mwanaspoti lilitafuta wadau ili kutoa mtazamo wao wa kiufundi.
Aliyekuwa kocha wa Tanzania Prisons, Aman Josiah alisema japo hawezi kuingilia majukumu ya mwingine kwa mtazamo wake, anayaona mambo mawili kikosi kipana ambapo Azam itacheza Ligi Kuu, Kombe la FA na michuano ya CAF, ili isije ikateteleka katikakati ya mashindano.
“Kitu kingine ninachokiona ni kubalansi timu kwa maana kocha akiamua kuswichi mfumo mfano akatumia viungo watatu mmoja atakuwa anaanzisha mashambulizi akitokea kwa kipa, hilo jukumu linaweza likafanywa na Mao, Meza ama Bajana, hivyo watamfanya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoshuka chini na kukaa eneo la kufunga mabao mengi ama kutoa asiti nyingi.”
Staa wa zamani wa Simba, Majimaji na Taifa Stars, Steven Mapunda alisema:”Ukiona katika nafasi moja kuna wachezaji wengi, yapo mambo mengi ambayo kocha anayaangalia, pia itamsaidia kuwa na kikosi kipana kulingana na timu atakazokutana nazo, mfano akikutana na timu inayoshambulia akijaza viungo itakuwa ngumu kupata matokeo.”
Mwingine aliyetoa mtazamo wake ni beki wa Yanga, William Mtendamema alisema:”Ninachokiona katika hilo Ligi Kuu ijayo itakuwa ngumu, mfano kocha akaamua kupanga viungo wengi akijua anakutana na timu pinzani inayoshambulia sana, itapata ugumu wa kufunga, pale kuna Mao, Bajana, Meza, Kanouté hao wote ni viungo wagumu na wanaweza wakapootezesha mashambulizi.”