Komba, wenzake wafungua kesi kupinga uchaguzi TFF

Wakili Alloyce Komba pamoja na wenzake watatu wamefungua kesi katika Mahakama Kuu wakipinga mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), unaotarajiwa kuhitimishwa Agosti 16, 2025 mjini Tanga.

Walioshtakiwa katika kesi hiyo ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT), TFF na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakidai kuwa mchakato huo umeendeshwa kinyume cha sheria na kanuni za michezo nchini.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa kesho, Alhamisi, Agosti 14, 2025, saa 3:00 asubuhi mbele ya Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Fatma Maghimbi.

Mbali na Komba, wadai wengine ni mawakili Jeremia Mtobesya, Deusdedit Luteja na Denice Tumaini. Miongoni mwa madai yao, wanaiomba mahakama kusitisha mara moja mchakato wa uchaguzi wa TFF hadi shauri lao litakapokamilika kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Ikumbukwe kuwa, mvutano kuhusu uchaguzi wa TFF umekuwa ukijitokeza mara kwa mara katika historia ya shirikisho hilo, hususan kuhusu uwazi na ushirikishwaji wa wadau.

Uchaguzi wa mwaka huu umeibua mjadala mpya baada ya malalamiko ya ukiukwaji wa taratibu, ikiwemo kushirikishwa kwa wagombea bila kufuata vigezo vilivyowekwa na BMT.

TFF ambayo ndiyo chombo kinachosimamia mpira wa miguu nchini kimekuwa kikifanya chaguzi zake kila baada ya miaka minne, lakini mara kadhaa mchakato wake umekumbwa na changamoto za kisheria, jambo linalotishia ratiba ya mashindano na mipango ya maendeleo ya soka.