Lissu, Jamhuri wagongana kuhusu kusomewa ushahidi wa uhaini mubashara

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu imeelekeza Jamhuri kuweka wazi ushahidi wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu Jumatatu ijayo, huku ukiibuka mvuatano ushahidi huo kurushwa mubashara.

Mahakama hiyo imetoa maelekezo hayo leo Jumatano Agosti 13, 2025 wakati kesi hiyo ilipotajwa na upande wa mashtaka ukaieleza mahakama hiyo kuwa tayari kesi hiyo imeshasajiliwa Mahakama ambayo ndio itakayosikiliza ushahidi dhidi yake na hatimaye kutoa hukumu.

Lissu anakabiliwa na kesi hiyo mahakamani hapo, Kisutu ilikofunguliwa kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu itakakosikilizwa katika hatua ya ushahidi na kuamuliwa.

Leo kesi hiyo ilipoitwa, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga ameieleza mahakama hiyo kuwa tayari wameshawasilisha hati ya mashtaka Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 262 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marejeo ya 2023.

Pia, Wakili Katuga amesema kuwa tayari kesi hiyo imesajiliwa Mahakama Kuu kwa namba ya usajili kuwa wa kesi ya jinai namba 19605 ya mwaka 2025.

Lissu alipopewa nafasi, ameuliza mahakama hiyo iwapo imeshapokea hati hiyo ya mashtaka iliyopelekwa Mahakama Kuu, kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu ili ajue kama anaendelea kusomewa maelezo ya mashahidi ya hilo shtaka la uhaini linalomkabili, au la.

“Kama file (jalada la kesi) limekuja kutoka Mahakama Kuu, tuendelee, mimi niko tayari”, amesema Lissu.

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chadema, Joseph Mbilinyi (kulia) akisalimiana na Kaimu Katibu Mkuu Chadema,John Mnyika, baada ya kuwasili kwenye Mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kusikiliza kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho,Tundu Lissu. Picha na Michael Matemanga

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga amesema kuwa kutokana na matumizi ya teknolojia kwa sasa taarifa (hati ya mashtaka) inapowasilishwa Mahakama Kuu ikapokewa na Msajili moja kwa moja inaingia kwenye jalada la mahakama ya chini.

“Kwa hiyo walipoisajili, mimi huku niliipata, ninaiona information (taarifa, yaani hati ya mashtaka) hapa kwenye file langu. Kwa hiyo hiyo information mlipoisajili Mahakama Kuu, baada ya Msajili kukamilisha utaratibu, nimeipata, kwa hiyo ipo hapa,” amesema Hakimu Kiswaga.

Mvutano ushahidi kusomwa na kurushwa mubashara

Baada ya majibu hayo ya Hakimu Kiswaga, Wakili Katuga amerejea uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri dogo la maombi namba 17059/2025, kuhusu ulinzi wa baadhi ya mashahidi wake katika kesi hiyo ambao ni raia.

Amesema kuwa maombi hayo yalilenga kutengeneza mazingira kwa mashahidi hao kutoa ushahidi wao bila kuathiriwa na vitisho walivyokuwa wanavipokea na kwamba nakala ya uamuzi huo imeambatanishwa kwenye hati ya mashtaka.

Wakili Katuga amesema Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilielekeza namna ya kuwalinda mashahidi hao wakati wa mwenendo kabidhi (committal proceedings) na wakati wa usikilizwaji kamili wa kesi hiyo (trial).

Amesema kuwa Mahakama Kuu kwa busara zake imesema kuwa hakutakuwa na chapisho la nyaraka yoyote au ushahidi wowote  utakaowezesha utambuzi wa mashahidi hao raia isipokuwa kwa ridhaa ya Mahakama Kuu.

“Msingi wa kuyasema haya ni kwamba shauri hili linaendeshwa na kurushwa moja kwa moja dunia nzima, kwa maana tayari tukiyasoma (maelezo ya mashahidi) kwa njia hii ya kurushwa moja kwa moja tumekinzana na uamuzi wa Mahakama Kuu,” amesema Wakili Katuga na kuongeza:

“Kwa hiyo mheshimiwa ombi letu sisi, pamoja na nia njema ya mahakama ya kuonesha moja kwa moja mwenendo wa shauri hili, tunaiomba mahakama yako tukufu iweze kufuata maelekezo katika uamuzi huu wa Mahakama Kuu kwa kuzuia uchapishaji wa namna hii.”

Wakili Katuga amefafanua kuwa kwa kusoma tu msingi wa ushahidi wa mashahidi hao hata bila kuwataja majina msingi wa ushahidi wao tu unaweza kusababisha kutambuliwa.

Hivyo ameomba mshtakiwa asomewe tu ushahidi huo katika mahakama ya wazi kama kifungu cha 263(2) cha CPA, 2023’  lakini usirushwe mubashara na vyombo vya habari kwani kufanya hivyo ni kukiuka amri ya Mahakama Kuu ya kutokuchapishwa nyaraka/ushahidi wa shahidi.

Hata hivyo, Lissu amepinga vikali maombi hayo ya Jamhuri kutaka ushahidi huo usirushwe mubashara, akidai kuwa kufanya hivyo ni kutaka kuingia katika utaratibu wa kuendesha kesi gizani, ikiwemo hiuyo yake ya uhaini ambayo adhabu yake ni kifo ili watu wasijue.

Lissu ameirejesha mahakama hiyo katika uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi hao akidai kuwa Wakili wa Serikali anataka kutanua amri ya Mahakama Kuu na kufunika hata yale ambayo Mahakama haikuyasema ili kila kitu kifanyike gizani.

Akisoma uamuzi huo amesema kuwa mahakama ilizuia utambulisho wao mashahidi wa Jamhuri yaani, majina, anuani na mahali wanapokaa katika mwenendo kabidhi na wakati wa usikilizwaji Mahakama Kuu.

Pia, amesema kuwa Mahakama Kuu imeelekeza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kuondoa katika nyaraka au ushahidi wao majina yao, maelezo, anuani na taarifa ambazo kwa kuziangalia tu zinaweza kufanya mashahidi wao wajulikane zitakaposomwa, sio kufunga televisheni na kuleta giza.

Vilevile amesema kuwa Mahakama Kuu imeelekeza kuwa wakati wa mwenendo kabidhi na usikilizwaji hakuna kusambaza wala kuchapisha ushahidi wowote wa nyaraka au ushahidi mwingine wenye utambulisho wa shahidi raia bila kwanza kuomba ridhaa ya  Mahakama.

“Hiyo maana yake kama wamefuta majina maelezo yao ya mahali walipo hiyo tayari utakuwa umeshaondoa kile ulichoelezwa usifanye. Kwa hiyo hoja kwamba mwenendo huu usitangazwe mubashara hiyo haijaamuliwa na Jaji,” amedai Lissu.

Hata hivyo, Wakili Katuga amefafanua kuwa licha ya kuondoa majina na taarifa nyingine za mashahidi hao, lakini kuna maelezo ambayo ndio msingi wa ushahidi haitakiwi kwenda hadharani kwani yanaweza kurahisisha mashahidi hao kujulikana.

Amesisitiza kuwa hawajaomba kesi isikilizwe chemba (bila watu wengine kuwepo) wala kuzuia watu kufika mahakamani bali wameomba ushahidi huo usomwe katika mahakama ya wazi isipokuwa tu usirushwe mubashara.

Akijibu hoja ya Lissu kuwa kutokurushwa mubashara ni kuendesha gizani, ameeleza kuwa hiyo ndio kesi ya kwanza nchini kurushwa mubashara na kwamba siku zote kesi zimekuwa zikiendeshwa katika mahakama ya wazi bila kurushwa mubashara lakini haijawahi kulalamikiwa kuwa zinaendeshwa gizani.

“Sisi tunasema publication (uchapishaji) iliyosemwa pale inahusisha livestream (matangazo ya moja kwa moja) na magazetini.

Akitafsiri mahakama ya wazi kwa mujibu wa kifungu cha 192, wakili Katuga amedai kuwa hakuna mahali kinasema mahakama ya wazi ni kuchapisha.

Akijibu tena hoja za Jamhuri, Lissu amesisitiza kuwa Mahakama Kuu haijazungumzia mambo ambayo hayafichiki, bali alikuwa wazi kabisa kuwa usitangaze wala kusambaza chochote ambacho kitafanya wajulikane na kwamba amefafanua kuwa  ni majina, anuani, makazi, mahali waliko.

Hayo yanajulikana, hayo ambayo Wakili wa Serikali anasema hayawezi kuzuilika ni yapi hayo ambayo Jaji Mtembwa hajayasema.

Amesema kuwa wanang’ang’ania matangazo mubashara kwa sababu inawezesha umma mkubwa kuelewa kinachoendelea hapa na kwamba kwa sababu hayo mengine Mahakama Kuu haijaamuru ni haki ya umma wote.

Amesisitiza kuwa anapigania haki ya uwazi na kwamba upande wa mashtaka unajua umma unafuatilia ndio maana wanataka giza, hivyo akasisitiza mahakama isiwakubalie.

Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo mpaka Agosti 18 kwa ajili kutoa amri kuhusiana na hoja hizo, huku akielekeza tarehe hiyo Jamhuri kusoma maelezo ya mashahidi wake.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka mola la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hili Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kuwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.