Mashujaa yajificha ufukweni Dar | Mwanaspoti

UNAITAFUTA Mashujaa? Basi usiende viwanjani kwani jamaa wako zao ufukweni wakizianza hesabu za kujipanga kwa ajili ya msimu ujao.

Wakiwa chini ya kocha mkongwe Salum Mayanga, Mashujaa wamekita kambi yao jijini Dar es Salaam, kujifua kwa mazoezi ya ufukweni.

Mashujaa wanafanya tizi wakikimbia mbio tofauti na mazoezi mengine ya fiziki, wakiwa kwenye fukwe za Msasani.

Ukienda huko utawaonea huruma wachezaji wa timu hiyo ambapo mmoja wa mastaa wapya, ameliambia Mwanaspoti kuwa ratiba ya mazoezi hayo ni magumu kiasi cha kuwaacha hoi huku usimamizi ukiwa mkubwa kutoka kwa makocha wa klabu hiyo.

“Huku sio mchezo ndugu yangu ni kama tunakwenda vitani, mazoezi haya ni makali sana, ukitoka unakuwa hoi kabisa unachotamani ni kupumzika tu,” alisema staa huyo.

Mazoezi hayo yanalenga kuimarisha pumzi kwa wachezaji wa timu hiyo inayotumia uwanja wa nyumbani unaojulikana kama Lake Tanganyika uliopo mkoani Kigoma.

Kama haitoshi ikimalizika ratiba hiyo ya ufukweni, kikosi hicho kinarudi kujifua jioni, wakihamia gym ambako nako kuna kazi nzito ya kutunisha misuli.

Mashujaa ikimaliza ratiba hiyo ya mazoezi ya ufukweni, itahamisha kambi yake na jijini Arusha kwa hatua ya pili ya maandalizi yao.

Bosi mmoja wa Mashujaa ameliambia Mwanaspoti kwamba, timu yao itakwenda huko kuendelea na maandalizi huku pia ikifuata fursa ya kucheza mechi za kirafiki.

Mbali na Mashujaa timu nyingine zilizoweka kambi Arusha ni pamoja na JKT Tanzania, Singida Black Stars na Azam FC.
Mashujaa ikijipanga na msimu ujao tayari imeshatangaza mastaa wake tisa waliosajiliwa katika dirisha hili la usajili wakiwamo:

1. Ismail Mgunda – Mshambuliaji
2. Frank Magingi – Beki
3. Mudathir Said – Mshambuliaji
4. Omary Omary – Kiungo
5. Mohamed Mussa – Beki
6. Kabasele Hamad – Beki
7. Sued Juma – Beki kushoto
8. Salum Kihimbwa – Mshambuliaji
9. Samwel Onditi – Kiungo