MAURTANIA inaendelea kuifukuzia Tanzania baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso na kuendelea kusalia nafasi ya pili kundi B la mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN 2024).
Ni mechi ya tatu ya kundi B iliyopigwa leo, Agosti 13, 2025, kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam bao la Maurtania likifungwa na Alassane Diop katika dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti.
Mchezo ulianza kwa timu zote kusaka bao la kuongoza, lakini hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza kabla ya tisa za nyongeza ambazo ndio bao lilipatikana, hakukuwa na mbabe licha ya Burkina Faso kucheza pungufu baada ya Patrick Bihetoue Malo kuonyeshwa kadi nyekundu.
Ushindi wa Maurtania unaifanya timu hiyo kufikisha pointi saba baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa mchezo mmoja huku Burkina Faso ikiendelea kubaki nafasi ya tatu na pointi tatu baada ya kushinda mechi moja na kufungwa mbili.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza matukio mengi yaliamuliwa na VAR kuanzia penalti, kadi nyekundu na hata maeneo tata ambayo faulo ilitakiwa kupigwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa mabadiliko kwa pande zote mbili, lakini hayakuwa na faida kwa Burkina Faso ambao licha ya kuwa pungufu iliweza kucheza mchezo mzuri kusaka bao la kusawazisha hadi dakika 90 za mchezo zinaisha ilishindwa kuambulia pointi.
Licha ya Burkina Faso kukosa bao la kusawazisha imeonyesha mchezo mzuri na wa ushindani ikiwapa wakati mgumu Maurtania timu ambayo ilikuwa mbele kwa bao la kuongoza.
Kwa matokeo hayo Maurtania inafikisha pointi saba na kuendelea kushika nafasi ya pili kwenye Kundi B ikiongozwa na Tanzania iliyo na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu na imebakiwa na mchezo mmoja.
Burkina Faso inabakiwa na pointi tatu ikibaki na mechi moja mkononi.