Serikali imesema inajipanga kuwa kitovu cha utengenezaji wa bidhaa na huduma migodini kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuvutia uwekezaji.
Hayo yameelezwa leo Jumatano, Agosti 13, 2025 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ambaye amesema hatua hiyo inalenga bidhaa na huduma hizo kwenye migodi ya ndani na nje ya nchi.
Waziri Mavunde alikuwa akizindua ghala la mauzo ya vipuri vya mitambo mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini linamilikiwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Shan Parts Africa ya India na Kampuni ya ITR ya Italy.
“Uamuzi wa kuwekezaji hapa Tanzania ni wa kupigiwa mfano, kwa hili nawapongeza sana kampuni za Shan Parts na ITR.
“Uwepo wa huduma hii nchini utapunguza kwa kiasi kubwa uingizaji wa vipuri kutoka nje na kupunguza gharama za uendeshaji.
Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu, kuwa na huduma kama hii itasaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya madini,” amesema Mavunde.
Amesema Serikali imetenga eneo la Buzwagi wilayani Kahama kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani na huduma migodini.
Hatua hiyo ya Serikali inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa na huduma migodini ya ndani na jirani.
Kwa upande wake, Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Ney na Balozi wa Italia, Giuseppe Coppola wamepongeza ushirikiano wa kibiashara wa mataifa hayo na kuahidi kuuendeleza.
Wamesema ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania, India na Italia ni mkubwa na unalenga kuendelea kukuza sekta ya madini ambayo ndio nyeti katika kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Shan Parts Africa Ltd, Malhar Dave amesema mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Rais Samia Samia Hassan yamewezesha kampuni hiyo kuwekeza hapa Tanzania.