Mkakati kuwawezesha bodaboda Dar wazinduliwa

Dar es Salaam. Shirikisho la vyama vya waendesha bodaboda Dar es Salaam (Maupida), wameweka mikakati inayolenga kuinua maisha ya watoa huduma hao wa usafiri kupitia mikopo nafuu, uwezeshaji wa mitaji na miradi ya makazi.

Mipango hiyo itakamilika baada ya kupatiwa cheti cha uwakala wa kukatisha leseni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhi (Latra) kwa bodaboda ambapo wanalipia Sh17,000 kwa mwaka na bajaji Sh22,000, huku asilimia 10 ya malipo hayo yakiingizwa kwenye Saccos ya bodaboda.

New Content Item (1)

Akizungumza leo Jumatano, Agosti 13, 2025 katika hafla ya kukabidhi cheti cha uwakala, Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Said Kagoma amesema awali benki zilikuwa zikitoa mikopo kwa riba ya asilimia 20, hali iliyokuwa inawadumaza wanachama wengi.

Amesema madereva wengi wamejikuta wakiingia kwenye madeni makubwa kutokana na gharama za upatikanaji wa pikipiki kutoka kwa watu binafsi wanaoingia nao mkataba, ambapo hupeleka Sh12,000 hadi Sh15,000 kwa siku ndani ya miezi 15 hadi 18.

“Baada ya majadiliano na uongozi wa wilaya (DC), walifanikiwa kushusha riba hiyo hadi asilimia 15, hatua iliyowezesha kuanza kununua pikipiki kwa bei nafuu,”amesema Kagoma.

Amesema kwa sasa, pikipiki ya magurudumu mawili inapatikana kwa kianzio cha Sh600,000 huku bajaji ikiwa ni Sh1.1 milioni kupitia mpango wa Saccos ya umoja wao.

“Saccos hii siyo tu ya kupata pikipiki, bali pia ya kujenga uwezo wa kifedha,” amesema Kagoma.

“Tunataka tuondokane na dhana ya kuishi kwa kubahatisha. Wanachama wetu wamiliki ardhi na nyumba,” amesema.

Kuhusu changamoto za kila siku barabarani, Kagoma amewataka waendesha bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka faini zisizo za lazima.

Amesema baadhi ya faini wanazolipa ni matokeo ya kutokufuata taratibu, na akasisitiza umuhimu wa kuvaa kofia ngumu (helmet), kubeba abiria kwa usahihi, na kuendesha kwa uangalifu.

Kagoma amesema kila shilingi inayolipwa kama faini ingeweza kusaidia kulipa mkopo au kununua mafuta hivyo amewataka madereva kufuata sheria

Hata hali, amewakumbusha baadhi ya wanachama kuhusu kuchelewesha marejesho ya mikopo na kuwataka kujipanga ili kuhakikisha mpango huo unaendelea bila vikwazo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesisitiza umuhimu wa waendesha bodaboda kuwekeza na kupanga mikakati madhubuti ya kiuchumi, ili kuepuka changamoto za kifedha na kuongeza usalama barabarani.

Mpogolo alieleza kuwa ushirikiano kati ya waendesha bodaboda na mamlaka za usafirishaji unawawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu ya wastani wa asilimia 10, ambayo inasaidia kulinda uchumi wa madereva na kuwasaidia kumudu gharama za maisha, ikiwemo upatikanaji wa bima za afya.

“Viongozi wa shirikisho la bodaboda na wengine hapa wamesema, kupitia makusanyo ya Saccos, madereva wanaweza kupata pikipiki kwa bei nafuu tofauti na soko la kawaida, kuongeza uwekezaji kwenye maduka ya spea, na kuboresha maisha yao kwa ujumla,” amesema Mpogolo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi udhibithi Usafiri wa Barabara kutoka Latra,  Johansen Kahatano amesema mamlaka hiyo imezindua mpango maalumu wa kubadilisha maisha ya madereva wa pikipiki kwa kuwapatia fursa ya kumiliki vyombo vyao vya usafiri, kupata leseni rasmi na huduma za kifedha kupitia ushirikiano na vyama vya ushirika.

Kahatano amesema mpango huo unalenga kuondoa changamoto za ajira zisizo rasmi, kuhakikisha usalama wa madereva na abiria, na kuongeza kipato cha vijana wanaojishughulisha na sekta hiyo.

“Tunataka madereva hawa wawe na ajira rasmi, wamiliki pikipiki zao, wawe na leseni na bima, na pia waendeshe biashara zao kwa kufuata sheria. Hii itasaidia kuboresha maisha yao na kupunguza vitendo vya uhalifu mitaani,” amesema Kahatano.