Musoma. Zaidi ya miradi 68 ya maendeleo yenye thamani ya Sh26.54 bilioni inatarajiwa kutembelewa, kukaguliwa na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu mkoani Mara, kuanzia Agosti 15 hadi 23, 2025.
Akizungumza leo Jumatano, Agosti 13, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema maandalizi yote yamekamilika na mwenge huo utapita katika halmashauri tisa za mkoa huo, ukigusa miradi ya elimu, maji, afya, miundombinu, utawala bora, mazingira na ustawi wa jamii.
Amesema ukiwa mkoani humo, Mwenge wa Uhuru pia utawashwa katika Mwenge wa Mwitongo, nyumbani kwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni kumbukumbu na ishara ya kumuenzi Baba wa Taifa.
“Ukiwa mkoani kwetu Mwenge wa Uhuru pia utapata fursa ya kuwasha Mwenge wa Mwitongo kule nyumbani kwa Mwalimu ambapo pamoja na mambo mengine mwenge huo ni kumbukumbu na ishara ya kumuenzi Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere,” amesema Kanali Mtambi.
Kanali Mtambi ameeleza kuwa mbio hizo zitahusisha umbali wa kilomita 1,122 kabla ya kukabidhi mwenge huo mkoani Mwanza, Agosti 24, 2025.
Baadhi ya wakazi wa Mara wamewahimiza wenzao kujitokeza kushiriki mbio hizo kwa wingi.
“Mwenge wa Uhuru unapokuja Mara ni kama umerejea nyumbani, tuonyeshe mapenzi yetu kwa Nyerere,” amesema Jonas Manyerere.
Kwa upande wake, Amina Ibrahimu amesema mwaka huu mbio hizo zinabeba ujumbe wa uchaguzi mkuu, hivyo ni fursa ya wananchi kupata ujumbe wa kauli mbiu ya “Jitokeze kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu.”