Dar es Salaam. Wakati Katibu wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Odero Charles akilalamikia kucheleweshwa kwa uamuzi wa tuhuma dhidi yake, uongozi wake umesema utakamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi huu.
Katika malalamiko yake, Odero amesema uongozi ukiendelea kukaa kimya ataamua kupambana na uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi unaoendelea.
Mzizi wa yote hayo ni taarifa ya Juni 30, mwaka huu ya viongozi wa kanda hiyo, waliotangaza kumsimamisha uongozi Odero, kwa walichoeleza walipokea malalamiko kuhusu mwenendo usioridhisha wa mwanachama huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Odero aliyewahi kugombea uenyekiti wa Chadema Taifa, katika uchaguzi uliofanyika Januari 21, 2025 alisimamishwa kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili. Hata hivyo, taarifa hiyo haikuweka wazi tuhuma hizo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatano Agosti 13, 2025, Odero amesema licha ya kusimamishwa kwake hadi sasa hakuna kinachoendelea ingawa anadai hajui sababu ya kuchukuliwa uamuzi huo ambao haujazingatia katiba ya chama hicho.
“Hakuna kinachoendelea na mimi nawasubiri, sitakuwa muongo au mpiga ramli, huwezi kumuandikia mtu barua ya kumsimamisha kwa sababu eti umepata tuhuma.
“Ni utaratibu ambao hauko sawa kikatiba na taratibu za chama chetu, bila kujiridhisha, uchunguzi hadi leo hkuna majibu na hakuna kinachoendelea, ni muhimu waseme wao kwa sababu wako kimya,” amesema.
Amesema kama viongozi wataendelea kukaa kimya atatumia kifungu cha 5.3.5 cha katiba ya chama hicho kuhusu wajibu wa mwanachama.
“Nipo tayari kupambana na namna yeyote ya uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi,” amesema Odero.
Alipoulizwa kuhusu sababu ya kusimamishwa kwake, amesema hajui chochote kwa kuwa hataki kuwa mpiga ramli anawasubiri.
Amesisitiza tangu alipotuhumiwa, hakuwahi kuitwa kusikilizwa kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Kanuni za chama hicho ya 6.5.5, 6.5.6 na 6.5.7.
“Kanuni hizo zinasema kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa mashtaka kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu mashtaka kwa maandishi.
Mbali na hiyo, Odero amefafanua ikiwa kuna makosa kiongozi husika zaidi ya utetezi wa maandishi, atapewa nafasi ya kujieleza bayana mbele ya kikao cha mamlaka ya nidhamu.
“Kanuni zetu zinasema kiongozi anayeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi ya maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumwezesha kuamua kukata rufani au la,” amesema Odero.
Akifafanua hatua ya uchunguzi ulipofikia, Katibu wa kanda hiyo, Totinan Ndonde amesema kutokana na michakato kwa kuzingatia kanuni za chama hicho, kushughulikia tuhuma zake ni sababu ya kuchelewa kutolewa uamuzi.
“Vikao vya kujadili suala lake vinatarajiwa kufanyika ndani ya mwezi huu na tutatoa taarifa. Si kwamba tuko kimya lazima tufuate zile taratibu na michakato ya kikatiba na kanuni za chama zinavyoelekeza,” amesema Ndonde.
Ndonde amesema hatua za awali wamekamilisha lakini kuna hatua mbili za kikatiba zinazopaswa kufuatwa kuanzia sasa.
“Baada ya uchunguzi kukamilika tuhuma zake zitapelekwa kwenye kamati tendaji ya kanda ikiangalia na kujiridhisha hoja za msingi za kujibiwa itaielekeza Kamati ya Maadili ya Kanda na baada ya hapo wataangalia kilichobainika,” amesema.
Kuhusu madai ya Odero kwamba hawajamsikiliza kabla ya kumsimamisha, Ndonde amejibu vyombo vyao vina nguvu kama Mahakama kwa maana ya kamati tendaji ya Kanda na kamati ya maadili.
“Kamati ya maadili ataitwa kuelezwa tuhuma zake na ajieleze hata akiwa na wakili ataruhusiwa kwenda kumtetea, akishajieleza majibu yake yataenda kamati tendaji nako ataitwa tena kujitetea na kujieleza,”amesema Ndonde.
Kulingana na unyeti wa tuhuma zinazomkabili, Ndonde amesema ndiyo maana walimsimamisha katika nafasi anayoshika ili isije ikaathiri uamuzi kwa vyombo vinavyopaswa kumchunguza na kuchukua hatua.
“Tumemsimamisha kuweka uwazi, haki na uamuzi utakaotolewa usionekane kuegemea upande wowote na ikiwa kuna hoja zenye mashaka zijibiwe kwa weledi,”amesema Ndonde.