Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe linawashikilia watuhumiwa watatu, akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji, kwa tuhuma za kumshambulia kwa kipigo kijana Ackrey Ngole (26), mkazi wa mtaa wa Maheve katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, wakimtuhumu kuiba matunda ya parachichi.
Taarifa hiyo imetolewa jana jioni, Agosti 12, 2025, na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Ally Kitumbu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya jeshi hilo mkoani humo.
Kwa mujibu wa Kamanda Kitumbu, tukio hilo lilitokea Agosti 9, 2025, katika mtaa wa Maheve, ambapo watu wanne walikamatwa na wananchi wakidaiwa kuiba parachichi, na miongoni mwao alikuwa ni kijana Ackrey Ngole.
Amesema baada ya jeshi hilo kuona picha za video zinazoonyesha kijana huyo akishambuliwa na watuhumiwa hao, hatua za haraka zilichukuliwa na watuhumiwa walikamatwa.
Kamanda Kitumbu ameongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, na baada ya kukamilika, watuhumiwa watatu watafikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
“Jeshi la Polisi baada ya kuona picha mjongea iliyoonyesha watuhumiwa wakimshambulia Ackrey Philipo Ngole lilichukua hatua za haraka ikiwa pamoja na kuwakamata watuhumiwa watatu ambao walionekana katika picha mjongeo wakishiriki kumchambulia kijana huyo,” amesema Kitumbi.
Amesema kijana aliyeshambuliwa na hali yake inaendelea vizuri baada ya kupelekwa hospitali na kupatiwa matibabu, huku akitoa onyo kwa watu kuacha kuendelea kujichukulia sheria mkononi pindi wanapokamata watuhumiwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo la parachichi mkoani humo limekuwa kivutio kikubwa, hivyo kuvutia uhalifu hivyo wale wanaojihusisha na kilimo hicho wahakikishe kwamba maeneo yao wanayaweka katika hali ya usalama ili isiwe kivutio kwa wahalifu.
Naye mkazi wa mji wa Njombe, Noby Swalle amesema vijana waache kuwa na tamaa ya fedha kwani inaweza kuwafikisha pabaya badala yake wafanye kazi halali ili kuweza kujipatia kipato.
“Watu pia waache kujichukulia sheria mkononi kwani ukifanya hivyo unaweza kuwa na wewe mtuhumiwa baada ya kumjeruhi au kusababisha kifo cha mtu,” amesema Swalle.